Gesi kutawala mjadala wa mafuta Afrika Mashariki

Dar es Salaam. Wachambuzi wa mambo wameeleza kuwa Mkutano na Maonesho ya 11 ya Petroli ya Afrika Mashariki (EAPCE’25) unaotarajiwa kuanza leo hapa nchini utaibua mjadala wa kuongezwa tafiti za gesi asilia.

Wamesema wakati dunia ikisukuma mbele agenda ya matumizi ya nishati safi, ni muhimu nchi za Afrika Mashariki kuangalia namna ya kuongeza matumizi ya gesi asilia kuachana na mafuta ambayo upatikanaji wake huhitaji fedha nyingi za kigeni.

Mkutano huo unatarajia kukutanisha washiriki zaidi ya 1,000, wakiwemo watunga sera, viongozi wa Serikali kutoka nchi mbalimbali hususani wa Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na wawekezaji wa ndani na wa kimataifa.

Naibu Waziri Mkuu Dk Doto Biteko ametoa wito kwa wawekezaji na wananchi kwa ujumla kutumia fursa ya Mkutano ujao wa Maonesho ya Petroli ya Afrika Mashariki 2025 (EAPCE’25) ili kupata ufahamu wa kina kuhusu Gesi Asilia Iliyobanwa (CNG) na faida zake.

Akizungumza katika kikao cha awali cha mkutano huo jana, Dk Biteko alisema kuwa mkutano huo haukuwa wa bahati mbaya bali ni tukio la wakati muafaka, linaloendana na juhudi za kimataifa za kubadili nishati kutoka kwa nishati hadi vyanzo safi vya nishati.

“Mpango wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wa kuanzisha Sera ya EAC ya Mabadiliko ya Tabianchi na Mpango Kabambe wa Mabadiliko ya Tabianchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ni uthibitisho wa wazi wa kujitolea kwa ukanda huu kushughulikia masuala ya tabianchi,” aliongeza.

Aliwataka washiriki kutumia mkutano huo kama jukwaa la kujadili mabadiliko kutoka kwa nishati ya mafuta hadi nishati safi Afrika Mashariki.

Kauli mbiu ya mkutano EAPCE’25 ambao Rais Samia Suluhu Hassan atakuwa mgeni rasmi ni “Kufungua fursa za uwekezaji katika nishati: Mchango wa rasilimali za mafuta katika kupata nishati ya uhakika kwa maendeleo endelevu ya Afrika Mashariki,”

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Huria Tanzania Dk Yohana Lawi amesema wakati dunia ikiwa katika hatua za mwisho za kuachana na matumizi ya petroli ni wakati sasa nchi za Afrika kujadili fursa kwenye gesi asilia na kuhimizwa kuongezwa kasi ya tafiti za nishati hiyo.

“Tuna muda mdogo wa kuendelea kutumia nishati chafu, tutumie rasilimali tulizonazo kuongeza tafiti zaidi, tayari Tanzania tumegundua gesi asilia futi trilioni 57.5 lakini bado hatujatumia kuchochea uchumi wetu,” amesema.

Dk Lawi amesema kwenye matumizi ya petroli nchi za Afrika Mashariki zinatumia fedha nyingi za kigeni kuagiza nishati hiyo jambo alilotafsiri ni kuyapunguzia mzigo nchi hizo za nishati zisizo hitajika.

“Hata mifumo ya magari kwa sasa inatengenezwa kutumia nishati safi, hivyo Tanzania ikiwa nchi ya mfano iharakishe usambazaji wa gesi asilia majumbani, kwenye magari na kuhakikisha mchakato wa vibali ili wawekezaji wajenge vituo vya mafuta maeneo mengi,” alisema.

Kitakachojadiliwa

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Felchesmi Mramba amesema mkutano huo utatoa nafasi ya kujadili mchango wa rasilimali za mafuta na gesi asilia katika mchanganyiko wa nishati kwa maendeleo endelevu ya Afrika Mashariki na fursa za uwekezaji zilizopo sekta ya mafuta na gesi Afrika Mashariki.

Mbali na hayo amesema mada mbalimbali kutoka kwa wataalam na wabobezi  sekta ya mafuta na gesi zitatolewa zikiwemo utafutaji na uendelezaji wa mafuta na gesi katika nchi za Afrika Mashariki,

Mada nyingine ni fursa za uwekezaji katika mnyororo wa thamani wa mafuta na gesi, dhana ya kuelekea nishati safi, masuala ya mazingira, miundo ya kisera, kisheria na kiudhibiti katika mafuta na gesi.

Fursa za mkutano

Mchambuzi wa masuala ya Uchumi Dk Mwinuka Lutengano amesema mkutano huo kufanyika nchini unaendelea kufungua fursa ya utalii wa mikutano.

“Hii imerudisha sifa yetu ya mikutano mikubwa kufanyika nchini, kwanza huu mkutano kufanyika vipo vigezo vimeangaliwa uwezo wa nchi yenyewe na usalama,” amesema.

Dk Lutengano amesema suala la usalama nalo limekuwa na mchango mkubwa wa mikutano mingi kufanyika nchini akidokeza sifa hizo zitavutia wawekezaji kuongezeka nchini.

Kuhusu uwekezaji amesema ujasiri wanaopata wawekezaji wanaofika kwenye mikutano hiyo utafanya kupata ujasiri wa kurudi kuwekeza kutokana na mazingira waliyoyaona.

Kwa upande wake Katibu wa Taasisi ya Wafanyabiashara wa Mafuta ya Rejareja Tanzania (Tapsoa), Augustino Mmasi alisema mkutano huo ni fursa ya kubadilisha uzoefu wa biashara ya mafuta kwa wawekezaji Afrika Mashariki.

“Mkutano huu utatusaidia kwenye uzoefu baina yetu wafanyabiashara lakini kuangalia ni fursa zipi tutazichangamkia ambazo zitajitokeza,” amesema.

Sababu mikutano kufanyika nchini

Profesa Abel Kinyondo mtaalamu a Uchumi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam amesema kufanyika kwa mikutano mingi ya kimataifa nchini ina maana kubwa kwa Tanzania.

“Tumerudisha hadhi tuliyokuwa nayo hapo mwanzoni ya kuvutia utalii wa mikutano mikubwa duniani, uwepo wa mikutano hii kwanza ni kutokana na uwepo wa ulinzi imara hapa nchini,

Pia inaonyesha Tanzania tuna miundombinu inayoruhusu mikutano hiyo kufanyika na Tanzania kuwa na marafiki wengi,” amesema.

Amesema miaka ya nyumba nchi ya Rwanda ndio ilianza kuvutia mikutano ya namna hiyo lakini Tanzania sasa imerejesha hadhi ya kuendesha mikutano hivyo ongezeko la mikutano kufanyika nchini ni jambo zuri.