
KOCHA mkongwe wa kikapu, Suleiman Tasso amesema anatarajia kuingiza timu mbili katika mashindano ya Ligi ya Kikapu Zanzibar, mwaka huu.
Akizungumza na Mwanaspoti, Tasso alizitaja timu hizo kuwa ni Zenji Bulls na Carvarious, ambapo Zenji Bulls haijacheza mashindano yoyote kwa kipindi kirefu.
Nilivyoiona timu hii kwa sasa imebadilika na wachezaji wamebadilika kutokana na viwango kupanda,” alisema Tasso
Akizungumzia maandalizi ya timu hizo, alisema yanakwenda vizuri katika viwanja vya mazoezi kila siku yanayofanyika katika Uwanja wa Mpendae uliopo mjini Unguja.
Aliwataja baadhi ya wachezaji nyota watakaoshiriki upande wa Zenji Bulls kuwa ni Amial Faki, Farid Nurdin, Suleiman Mohamed na Issa Omary, ilhali upande wa Carvarious ni Abdul Salim, Kassim Hamid, Nabir Abdi na Omary Tasso.
Akizungumzia kuhusiana na mchezo wa kikapu wa wheelchair, Tasso alisema wanaendelea kuhamasisha uchezwe eneo lote la Zanzibar ili kushawishi na kuwafanya watu wenye ulemavu kuhamasika kuupenda na kuanza kuucheza.
Alisema tayari kuna wachezaji 25 wa wheelchair anaowafundisha na wameanza kucheza.
“Tumekuwa tukitembelea viwanja mbalimbali, tukicheza wenyewe kwa wenyewe huku tukiwaalika watu wenye ulemavu waje kujifunza mchezo huo unavyochezwa,” alisema Tasso.