
Dar es Salaam. Jumla ya Sh64.3 milioni zimekusanywa kupitia operesheni ya ‘Tone Tone’ inayoendeshwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa siku 16 kuanzia Februari 12 hadi Machi 1, 2025.
Licha ya shughuli ya uchangishaji fedha hizo kwa mfumo wa dijitali kuanza Februari 12 lakini operesheni hiyo ilizinduliwa rasmi na mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu Februari 27, 2025 hafla iliyohudhuriwa na makada na viongozi wengine waandamizi wa chama hicho akiwamo, Makamu Mwenyekiti Bara, John Heche, Katibu Mkuu, John Mnyika.
Msingi wa kukusanya fedha hizo ambazo chama hicho kimejiwekea lengo la kukusanya Sh1 bilioni kwa miezi sita, zinalenga uendeshaji wa chama hasa kupita kutoa elimu nchi nzima kushinikiza madai ya mifumo huru ya uchaguzi kupitia kampeni yao ya ‘No reform no election.’
Akizungumza katika mkutano na vyombo vya habari uliofanyika makao makuu ya Chama hicho, Mikocheni Dar es Salaam leo Jumatatu, Machi 3, 2025 Naibu Katibu Mkuu wa Chadema-Bara, Amani Golugwa amesema kamati ndogo ya fedha inayosimamia ukusanyaji huo ikiongozwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama hicho, Godbless Lema itakuwa inatoa mrejesho kila baada ya siku saba.
“Fedha walizochanga Watanzania kupitia Tone Tone kuanzia Februari 12 baada ya Mwenyekiti kuzungumza kupitia njia mbalimbali ni Sh64.3 milioni. Tunawashukuru wa Tanzania kwa moyo huu niwaahidi tutakuwa wawazi kwa kila mnachokituma,” amesema.
Kulingana na maelezo ya Golugwa amesema mgawanyo wa namna fedha hizo zilivyokusanywa ni kupitia akaunti ya NMB ni Sh16.8 milioni mbali na njia hiyo kupitia namba ya mtandao wa Mpesa zimechangwa Sh39.9 milioni.
“Kupitia njia ya Mpesa bili jumla ya Sh5.7 milioni Watanzania wamedondosha matone madogo madogo hadi kufikisha kiwango hiki lakini kwa njia ya Mixx bili Sh1.7 Milioni na kufanya jumla tumekusanya jumla ya fedha Sh 64.3milioni,” amesema.
Golugwa amewashukuru Watanzania kwa kuendelea kuwaamini na kufanyikisha kuchangisha kiwango hicho cha fedha.
Changamoto
Mbali na mafanikio hayo, Golugwa amekiri kukutana na changamoto katika mifumo ya ukusanyaji fedha hizo kwa baadhi ya namba lakini wanaendelea kuwasiliana na mamlaka kuona mambo yanaenda vizuri.
“Wachangiaji wengi wa Tone Tone walipata changamoto na kwa jinsi watu walivyojisajili kwetu, tunaamini kiwango kinaweza kuzidi Sh150 hadi Sh200 milioni zilizokusanywa kwa sababu wachangiaji wengi walikuwa wanakataliwa mfumo umejaa hata wakiwa na fedha kidogo,” amesema.
Katika kutatua changamoto hiyo tayari wameshawasiliana na mamlaka zinatatuliwa na kuwasihi Watanzania waendelee kudondosha matone madogo madogo.
“Tunataka kila Mtanzania aweze kushiriki na kusudio letu chama kirudi kwenye mikono ya watanzania wenyewe, wakiendeshe na tunaamini hata viongozi tutalazimika kuwajibika kwa watu,” amesema.
Golugwa amesema kwa namna Watanzania wanavyoendelea kuchanga wataendelea kuwa wanyenyekevu na kuwajibika kwa jamii katika kuhakikisha wanapigania haki za watanzania.
“Fedha hizi ambazo Watanzania mnazitoa na ambazo mnaendelea kuzitoa zitafanya kazi ya kutuwezesha tuliokuwa wachache na wengi waliopo uko kuungana kama gharama ya kuwafikia mahali popote Tanzania na tutahitaji kuweka mafuta kwenye magari na kuandaa mikutano ya kutoa elimu,” amesema.
Amesema viongozi wa chama hicho ngazi ya majimbo watahitaji fedha kwa ajili ya kufanya mikutano ya hadhara katika maeneo yao na zitatumika kwa mfumo huo.
“Tunawaahidi kila baada ya siku saba tutakuwa tunatoa taarifa ya mrejesho ya mapato njinsi ambayo Watanzania mnatoa fedha zenu na kuzichanga na mtajua jinsi zinavyotumika,” amesema.
Baada ya kukusanya fedha hizo wanatarajia kuanza kufanya mikutano ya kudai mifumo ya uchaguzi kanda ya Kusini kwa mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi.
“Siku 48 tutakuwa barabarani kuanzia nyanda za juu kusini tutakuwa tunafanya mikutano ya hadhara kutoa elimu nini maana ya no reform no election, fedha hizi zinatumika na wapambanaji waliojitolea kudai haki yetu,” amesema.
Akizungumza siku ya uzinduzi wa operesheni hiyo, Tundu Lissu amesema uongozi wa chama hicho unajukumu kubwa mbele yao na ili wakamilishe lengo la kuikomboa nchi ni lazima waungwe mkono kwa kuwachangia.
“Tunahitaji ukombozi na ili tufanikiwe tunahitaji kuungwa mkono kwa kila mmoja kuchanga kidogo kidogo tuweze kukusanya fedha zitakazotuwezesha kuzunguka nchi nzima kufanya mikutano ya kutoa elimu ya kudai haki,” amesema.