Sh500 milioni kuchangishwa kusaidia watoto wenye miguu kifundo

Dar es Salaam. Wadau wa afya wakishirikiana na Hospitali ya CCBRT wameingia makubaliano ya kuchangisha Sh500 milioni ili kusaidia matibabu ya watoto 400 kati ya 1,000 wanaoendelea na matibabu ya tatizo la miguu kifundo (clubfoot) kila mwaka hospitalini hapo.

Hayo yamesemwa leo Machi 3,2025 na Mtaalamu wa Kitengo cha Mifupa hospitalini hapo, Frank Arabi katika hafla ya utiaji saini wa makubaliano baina ya  hospitali hiyo na GSM Foundation, Wizara ya Afya na Klabu ya Mpira Dar Young African ili kuwasaidia watoto 400 wenye tatizo hilo.

“Tatizo la miguu kifundo ni la kuzaliwa nalo, miguu ya mtoto hugeukia nyuma, na matibabu ya tatizo hili huanza wiki mbili baada ya kuzaliwa mpaka kufikia miaka 5,” amesema.

Arabi amesema, hatua ya kwanza ya matibabu ya tatizo hilo, huanza kwa mtoto kuvalishwa hogo (POP) akiwa na umri wa wiki sita mpaka mwezi mmoja.

“Baada ya mwezi kuisha, mtoto huvalishwa kiatu maalumu ambacho ni moja ya matibabu na atakivaa mpaka atakapofikisha miaka mitano,”amesema.

Pia, amesema kiatu hicho hubadilishwa kipimo kadri mtoto anavyokua.

“Mbali na kutibu watoto wachanga wenye tatizo hilo, tunapokea pia watoto wenye umri wa miaka saba, tiba pekee ni upasuaji,”ameeleza Arabi.

 Mkuu wa GSM Foundation, Faith Gugu amesema taasisi hiyo imeandaa hafla ya kuchangisha fedha kupitia futari maalumu katika mwezi Mtukufu wa Ramadhan.

“Tunaamini kila mtoto anastahili fursa ya kutembea, kukimbia na kufanikisha ndoto zake,” amesema.

Faith amesema, kilele cha harambee hiyo, kitakuwa Machi 14, 2025 katika ukumbi wa Super Dome Masaki.

Aidha, Johnson Amon mzazi wa mtoto mwenye tatizo la miguu kifundo amesema mwanaye ameanza matibabu akiwa na miezi mitano.

“Ndugu waligundua mtoto kuwa na tatizo akiwa Tanga na ndipo niliagiza aletwe Dar es Salaam ili apate matibabu,” ameeleza.

Amon amesema alipofika hospitalini hapo alitarajia huduma zitakuwa bure kutokana na kuwepo kwa wafadhili wa matibabu hayo.

“Japo nilikosa wadhamini ilibidi nitoe pesa ya matibabu,”ameeleza

Amesema, tangu waje hospitali ni wiki ya sita sasa.

Mwakilishi wa Wizara ya Afya ambaye pia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Magonjwa Yasiyoambukiza, Dk Omary Ubuguyu ametoa shukurani kwa wadau hao na kuongeza kuwa, ni vyema tukio la uchangishaji likafanyika pia Machi 8, 2025.

“Kwa kuwa tukio hili ni la kila mmoja, nashauri pia lifanyike siku ya Dabi ya Yanga na Simba ili kufikia kiasi kilichopangwa.”