
Mkuu wa Majeshi ya Uganda (CDF), Jenerali Muhoozi Kainerugaba, amewasili nchini Rwanda Jumapili kwa mkutano wa hadhi ya juu na Rais Paul Kagame.
Imechapishwa:
Dakika 2
Matangazo ya kibiashara
Muhoozi mapema wiki hii iliyopita alifichua mipango ya kusaini Mkataba wa Ulinzi kati ya Uganda na Rwanda.
Muhoozi, mshirika wa karibu wa Kagame, alitoa tangazo hilo kabla ya safari yake kwenye mtandao wa kijamii wa X, ambapo alitangaza kuwa Uganda na Rwanda zitasimama pamoja dhidi ya vitisho vyovyote.
“Nikiwa Kigali, nitatia saini pia Mkataba wa Ulinzi kati ya Uganda na Rwanda,” Muhoozi alisema.
“Mtu yeyote anayeshambulia nchi yetu yoyote atakuwa ametangaza vita dhidi ya nchi zote mbili,” aliongeza, kabla ya kuondoka kuelekea Kigali.
Ziara ya Muhoozi inafuatia mfululizo wa mikutano ya ngazi ya juu ya usalama kati ya Uganda na Rwanda, ikiwa ni pamoja na mkutano wa hivi karibuni wa usalama wa mipakani uliofanyika Mbarara, Uganda, Februari 27, 2025, ambapo wawakilishi kutoka mataifa yote mawili walijadili juhudi za kuimarisha ushirikiano wa kiusalama na kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na watu kati ya nchi hizo mbili.
Mkutano wa usalama wa Mbarara ulichukua jukumu muhimu katika kuunda ushirikiano wa kijeshi unaoendelea kati ya Uganda na Rwanda.
Mkutano huo uliohudhuriwa na Meja Jenerali Mstaafu Robert Rusoke, Balozi wa Uganda nchini Rwanda, na Balozi Vincent Karega, Mjumbe wa Rwanda katika Ukanda wa Maziwa Makuu, ulilenga masuala ya usalama wa mipakani, uhamiaji, biashara, forodha na uwekaji mipaka.
Ziara ya Muhoozi pia inakuja wakati ambapo mvutano umeongezeka katika eneo la Maziwa Makuu, hususan mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ambapo waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda wameteka maeneo muhimu, na kitendo hiki kulaaniwa katiak ngazi ya kimataifa.
Mahusiano
Mkataba wa Ulinzi kati ya Uganda na Rwanda, utakapokuwa rasmi, unatarajiwa kuimarisha ushirikiano wa kijeshi kati ya nchi hizo mbili, ambazo zimekuwa na historia ngumu ya ushindani na ushirikiano katika eneo hilo.
Tamko la Muhoozi kwamba “mtu yeyote atakayeshambulia nchi yetu yoyote atakuwa ametangaza vita dhidi ya nchi zote mbili” inaashiria mabadiliko makubwa katika ushirikiano wa kijeshi wa kikanda, hasa wakati kuna shinikizo kutoka nchi za Magharibi kwa Rwanda kuondoa wanajeshi wake katika ardhi ya DRC.
Wakati Rais wa Uganda Yoweri Museveni amejizuia hadharani kuungana na Rwanda katika mzozo unaoendelea DRC, Muhoozi-ambaye amezidi kuchukua nafasi huru ya kisiasa na kijeshi-ameunga mkono waziwazi uongozi wa Kagame na kudokeza mbinu ya kuingilia kati zaidi katika masuala ya kikanda.
Uganda, ambayo ina operesheni za kijeshi mashariki mwa DRC kwa kisingizio cha kupambana na waasi wa Allied Democratic Forces (ADF), haijajiunga rasmi na waasi wa M23.