WPL kuipisha Samia Women Super Cup

LIGI Kuu ya Wanawake (WPL) inatarajiwa kusimama kwa takriban wiki moja kupisha michuano ya Samia Women Super Cup inayotarajiwa kuanza kesho, kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.

Ligi hiyo iliyotarajiwa kurudi Machi nne baada ya mapumziko ya kupisha michuano ya kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (Wafcon 2026) Morocco, sasa itarudi Machi 12 na timu zote zitacheza siku hiyo.

Timu zilizoko nafasi nne za juu kwenye ligi hiyo, ndiyo zinazoshiriki michuano hiyo itakayopigwa kwa siku tatu, Machi 4 hadi 7 ambazo ni Simba Queens, JKT Queens, Yanga Princess na Fountain Gate Princess ambayo inashiriki badala ya Mashujaa iliyo nafasi ya nne kutokana na kuwa kwenye mkoa unaoandaa michuano hiyo.

Mchezo wa kwanza wa nusu fainali utazikutanisha Simba na JKT, huku nusu fainali ya pili Yanga itakutana na Fountain Gate Princess.

Ratiba ya awali ilionyesha baada ya mapumziko ya mashindano ya WAFCON yaliyoishia Februari 27 huku Timu ya Taifa ‘Twiga Stars’ ikivuka raundi ya pili baada ya kuitoa Equatorial Guinea kwa jumla ya mabao 4-2 itaanza Machi 04 kwenye muendelezo wa raundi ya 13.

Ligi hiyo ikirudi kwa raundi ya 13, Mashujaa Queens itakipiga na JKT Queens (Maj Gen Isamuhyo), Alliance Girls v Gets Program (Nyamagana),Bunda Queens v Fountain Gate Princess (Karume),Mlandizi Queens v Ceasiaa Queens (TFF Centre Kigamboni) na Simba Queens v Yanga Princess (KMC).