Msigwa: Waviu walitaka dawa za miaka miwili wakihofia kukosa ARV

Dar es Salaam. Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa amesema baada ya kutangazwa kusitishwa kwa misaada kutoka Marekani, baadhi ya watu wanaotumia dawa za kufubaza makali ya virusi vya Ukimwi (ARV) walifika vituo vya afya na kuomba kupewa dawa za miaka miwili hadi mitatu.

Hiyo ilitokana na hofu iliyokuwa imejengeka miongoni mwao juu ya hali itakavyokuwa pindi dawa wanazotumia zitakapoachwa kuletwa.

Msigwa ameyasema hayo leo Machi Mosi, 2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari alipokuwa akitoa mrejesho wa ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan mkoani Tanga, mrejesho wa mkutano wa tatu wa nchi zinazozalisha kahawa na uwasilishaji wa miaka minne ya Samia madarakani.

Akizungumza na wanahabari, Msigwa amewatoa hofu waviu juu ya hali ya upatikanaji wa dawa huku akisema Serikali imejiandaa vya kutosha kama fedha za wadau zitakatika, basi dawa hizo zitanunuliwa na kugawiwa kwa wahusika.

“ARVS zipo, Watanzania mnaotumia dawa ishini kwa amani, chapeni kazi na muendelee kuchukua tahadhari ya kutoambukiza wengine. Dawa zipo, Serikali yenu ipo itawaangalia na hatutoishiwa na hamtakosa dawa,” amesema.

“Sasa ukizichukua hizo dawa ukaenda kuziweka nyumbani zitaharibika, zikiharibika hazitakusaidia zitakuletea shida kwenye afya, acheni zikae kwenye vituo zinakohifadhiwa vizuri na nyie fuateni utaratibu mnaopewa na wataalamu wa kwenda kupokea dawa kama mlivyopangiwa,” ametoa wito.

“Mpo salama chapeni kazi, tuendelee kutekeleza afua zote za kukabiliana na maambukizi ya virusi vya Ukimwi. Niwaombe vijana wenzangu kuchukua tahadhari Ukimwi bado upo, tujikinge ili tuumalize, dunia ya sasa inazungumza kuumaliza Ukimwi na sisi Watanzania tuwe wa kwanza,” amesema.

Januari 28 mwaka huu, Rais wa Marekani, Donald Trump aliagiza kusitishwa usambazaji wa dawa za Ukimwi, malaria na kifua kikuu kwa nchi zinazopewa misaada na Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID).

Hatua hiyo ililenga kupitia upya miradi mbalimbali ya misaada jambo ambalo liliibua wasiwasi mkubwa miongoni mwa wataalamu wa afya na mashirika ya kibinadamu.

Kwa mujibu wa duru za kimataifa, agizo hilo linatarajiwa kuathiri mamilioni ya watu wanaotegemea huduma za matibabu kupitia programu kama Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na Ukimwi (PEPFAR).

Mpango huo, ulioanzishwa mwaka 2003, umeokoa zaidi ya maisha ya watu milioni 25 barani Afrika.

Aidha, mashirika yanayotoa msaada, likiwamo la Chemonics, yamesema hatua hiyo itavuruga upatikanaji wa dawa na huduma kwa watu walioko hatarini zaidi.