
Dar es Salaam. Kumbukumbu mbili zisizovutia zinailazimisha Coastal Union kuhakikisha inapambana kupata pointi tatu katika mchezo wake wa nyumbani dhidi ya Simba leo kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
Ya kwanza ni ya kutofanya vizuri katika mechi zake 10 zilizopita za Ligi Kuu ambapo imepata ushindi mara mbili tu, ikitoka sare sita na kupoteza mechi mbili.
Nyingine ya pili ni unyonge ambao imekuwa nao dhidi ya Simba ambapo mara nyingi ambazo timu hizo zinakutana kwenye Ligi Kuu, Coastal Union imekuwa ikipoteza na mara chache ikipata pointi kwa kutoka sare au ushindi.
Katika mechi 12 zilizopita za Ligi Kuu baina ya timu hizo, Simba imeibuka na ushindi mara tisa na mara tatu zimetoka sare.
Safu ya ushambuliaji ya Coastal Union imeonekana kuiangusha timu hiyo katika siku za hivi karibuni jambo ambalo linailazimisha leo ifanye kazi ya ziada ili iweze kutimiza malengo ya ushindi.
Timu hiyo inayonolewa na kocha Juma Mwambusi, katika mechi tano zilizopita imefunga bao moja tu wakati huo safu yake ya ulinzi ikiwa imeruhusu mabao manne.
Inakutana na Simba ambayo imekuwa na takwimu nzuri hasa katika safu yake ya ushambuliaji ambayo imefunga bao katika mechi 14 mfululizo na katika mechi tano zilizopita imefumania nyavu mara 12 ikiwa ni wastani wa mabao 2.4 kwa mchezo.
Timu hizo zinakutana zikiwa na kumbukumbu ya kutoka sare ya mabao 2-2 katika mechi ya mwisho baina yao iliyochezwa katika Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, Oktoba 4, 2024 ambayo zilimaliza kwa sare ya mabao 2-2, mabao ya Simba yakifungwa na Mohammed Hussein na Leonel Ateba huku mabao ya Coastal Union yakipachikwa na Ernest Malonga na Abdallah Hassan.
Kocha msaidizi wa Simba, Seleman Matola amesema kuwa mchezo huo wa leo utakuwa mgumu.
“Hakuna mechi rahisi na mzunguko wa timu kila timu ipo vizuri inataka pointi tatu.na waliokuwa chini wanataka kuja juu na tuliokuwa tupo juu tunatafuta ubingwa. Hautokuwa rahisi lakini tutahakikisha tunapata matokeo katika mchezo wa kesho (leo),” amesema Kapombe.
Kocha wa Coastal Union, Juma Mwambusi amesema kuwa pamoja na kutopata muda wa kutosha wa kupumzika, watajitahidi kupata ushindi leo.
“Tunajua mechi itakuwa ngumu na yenye ushindani mkubwa kwa sababu kama Coastal Union tumeshajipanga tupo tayari kuukabili mchezo huo. Tunajua wenzetu wametoka kupata pointi moja kama sisi vilevile tulivyopata pointi moja Namungo.
“Hatupo kwenye nafasi nzuri sana, tunahitaji kutoka hapa tulipo na kusogea katika nafasi za juu zaidi ambazo Coastal Union tunastahili kuwepo,” alisema Mwambusi.