Kibaha. Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali (CAG), Charles Kichere amesema mkakati wa serikali kwa sasa ni kuona mashirika ya umma nchini yanajiimarisha kiuchumi ili yajiendeshe bila kutegemea ruzuku ya serikali.

Amesema mbali na kujitegemea, pia mashirika hayo yanapaswa kujiwekea utaratibu wa kupeleka gawio la faida yatakayokuwa yanazalisha serikalini kila mwaka, hali itakayosaidia kukuza uchumi na maendeleo ya nchi.
Kichere ameyasema hayo jana Jumatano February 26,2025 Kibaha mkoni Pwani wakati akifunga kikao kazi cha siku mbili kinachowahusisha watendaji wa ofisi ya msajili wa hazina na ofisi ya Taifa ya mkaguzi wa hesabu za Serikali kilichokuwa na lengo la kuweka mikakati ya kuboresha utendaji kazi.
“Lengo kuu la kikao kazi ilikuwa ni kubadilishana uzowefu na kuhakikisha mashirika ya umma yanajiendesha kwa faida ili yabadilishe mtazamo wa kutegemea ruzuku serikalini na badala yake yenyewe yapate faida na kutoa gawio kwa serikali,” amesema Kichere.

Amesema iwapo watumishi wa mashirika hayo watajikita katika matumizi ya teknorojia katika utendaji wao wa kazi, wataimarisha uwazi na uwajibikaji na hatimaye kufikia malengo tarajiwa.
Kwa upande wake, Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu amesema malengo makuu ya mashirika kwa sasa ni kuweka mikakati ya kufikia maono ya serikali ya mwaka 2050.
“Tunataka mabadiliko ya kiutendaji na ili yote yafanyike yanahitaji usimamizi bora na utendaji bora na katika hilo tumeona tukutane pamoja ili kuweka mikakati muhimu,” amesema Mchechu.
Amesema iwapo mashirika ya umma yatatekeleza mikakati iliyofikiwa kwenye kikao kazi hicho cha siku mbili yatakuwa na uwezo wa kujiendesha kwa tija na hata kutoa gawio serikalini.
Agost 2024 Rais Samia Suluhu Hassan akiwa Mjini Arusha wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha wenyeviti wa bodi na watendaji pamoja na wakuu wa Taasisi,na mashirika ya umma kilivhofanyika kwenye kituo cha mikutano cha kimataifa (AICC), aliyataka mashirika ya umma kupunguza utegemezi serikalini katika utendaji wao.
Kiongozi huyo wa nchi aliwataka viongozi wa mashirika hayo kuimarisha utamaduni wa uajibikaji na kuhakikisha matumizi bora ya fedha za umma.