Baresi atimuliwa usiku usiku na Mashujaa

Kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa Singida Black Stars jana Jumatano, Februari 26, 2025 kimeondoka na kocha wa Mashujaa, Mohammed Abdallah ‘Baresi’.

Saa sita kasoro usiku ikiwa ni saa chache baada ya matokeo hayo, uongozi wa Mashujaa FC umetangaza kuachana na Baresi na wasaidizi wake.

“Uongozi wa Klabu ya Mashujaa Fc unapenda kuutarifu umma kuwa umefikia makubaliano ya kuvunja mkataba na kocha mkuu Mohamed Abdallah ‘Baress’.

“Vilevile Uongozi wa Mashujaa Fc umesitisha mkataba wa kocha wa viungo Hussein Bunu pamoja na kocha wa makipa Rafael Nyendi.

“Kwa sasa timu itakuwa chini ya kocha msaidizi Charles Fredie wakati mchakato wa haraka wa kumpata kocha mkuu ukiendelea.

“Uongozi wa Klabu unapenda kuwashukuru makocha hao kwa mchango wao dani ya Klabu yetu na unawatakia kila la kheri katika majukumu yao mapya,” imefafanua taarifa ya Mashujaa.

Baresi ameonyeshwa mlango wa kutokea akiwa ameiongoza timu hiyo katika mechi 22 za Ligi Kuu ikikusanya pointi 23 ambapo imepata ushindi mara tano, imetoka sare nane na kupoteza mechi tisa.

Kocha huyo hadi anavunjiwa mkataba na Mashujaa FC, alikuwa ndiye kocha aliyedumu kwa muda mrefu zaidi kwenye timu moja katika ligi.

Baresi aliiongoza Mashujaa msimu wote uliopita ambapo aliiwezesha kusalia kwenye Ligi Kuu na pia kufika hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB.