
Rome. Papa Francis ametimiza siku 12 akiwa amelazwa hospitali kwa matibabu, muda ambao ni mrefu ikilinganishwa na mwaka 2012 ambapo alilazwa kwa siku 10.
Kulazwa hospitali kwa Papa Francis kwa siku 12 ni muda mrefu zaidi wa kulazwa hospitalini tangu alipochaguliwa kuwa Papa.
Kabla ya ugonjwa unaomsumbua sasa, Papa Francis aliwahi kulazwa kwa siku 10 katika Hospitali ya Gemelli huko Roma mwaka 2021, baada ya kufanyiwa upasuaji wa utumbo mkubwa.
Tangu alipolazwa katika Hospitali ya Agostino Gemelli mjini Roma Ijumaa, Februari 14, 2025, akisumbuliwa na ugonjwa wa ‘bronchitis’, hali ya afya yake imekuwa ya kubadilika badilika, japokuwa madaktari wanaomtibu walidai kuwa hali yake siyo ya kutia hofu.
Kwa sasa, Papa Francis anapokea matibabu ya nimonia inayoshambulia mapafu yote mawili, huku matibabu ya changamoto ya dalili za awali za figo zake kufeli yakionekana kuleta mafanikio.
Ofisi ya Habari ya Vatican (Holy See) imesema pamoja na kuwa Papa Francis bado yuko mahututi ila afya yake inaendelea kuimarika huku ikidokeza kuwa amelala kwa utulivu usiku wa kuamkia leo.
Taarifa ya Vatican kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo Jumatano Februari 26, 2025, imesema: “Papa alilala kwa utulivu usiku na anaendelea kupumzika,”
Taarifa ya Jumanne jioni kuhusu afya ya Papa ilieleza kuwa hali ya kiafya ya Papa Francis bado ni mahututi japo ni thabiti, huku ikidokeza kuwa hakukuwa na tishio lolote la kumfanya apumue kwa shida.
“Jioni, alifanyiwa uchunguzi wa kipimo cha ‘CT-scan’ kama ilivyopangwa ili kufuatilia hali ya maambukizi ya nimonia katika mapafu yake. Bado tahadhari juu ya afya yake ni ya hali ya juu,” imeeleza taarifa hiyo.
Vatican pia kupitia taarifa hiyo imesema leo (Jumatano) asubuhi, Papa Francis baada ya kupokea Ekaristi takatifu aliendelea na shughuli zake za kikazi.
Jioni ya Jumapili, madaktari walisema vipimo vya damu vilionyesha dalili za awali za figo zake kufeli, lakini hali hiyo imeendelea kudhibitiwa. Walisema kwamba Papa bado yuko katika hali mahututi, lakini hajapata shida zaidi ya kupumua tangu Jumamosi usiku.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Associated Press (AP), Papa Francis (88), jana jioni alimpigia simu kasisi wa parokia ya Gaza nchini Palestina.
Pia, alitoa shukrani zake kwa watu wote wa Mungu waliokusanyika kusali kwa ajili ya kuombea afya yake katika siku za hivi karibuni.
Papa, ambaye aliwahi kuondolewa sehemu ya pafu lake alipokuwa kijana, aliongezewa damu mara mbili Jumapili ili kuongeza kiwango cha hemoglobini.
Tishio kubwa zaidi kwa Papa, kwa mujibu wa madaktari ni ‘sepsis’ ambayo ni maambukizi hatari ya damu yanayoweza kutokea kama tatizo linalotokana na nimonia.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.