
Dar es Salaam. ‘Ilianza kufunga Azam na kumalizia wao’ ndivyo unavyoweza kusema baada ya kuipunguza Simba kasi kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu baada ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2.
Mchezo huo wa 20 kwa Simba na 21 kwa Azam umechezwa leo Februari 24, 2025 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Azam ndio imekuwa ya kwanza kupata bao katika mchezo huo kupitia kwa Gibril Sillah katika dakika ya pili ya mchezo akimalizia mpira uliotemwa na kipa Mousa Camara.
Baada ya kuingia bao hilo, timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu, Simba ikitumia soka la pasi huku Azam ikicheza kwa kutegemea mashambulizi ya kushtukiza.
Mbinu ya Simba ndio ilionekana kuzaa matunda baada ya dakika ya 26 ikapata bao la kusawazisha kupitia kwa Elie Mpanzu.
Mpanzu alifunga bao hilo akimalizia pasi ya Kibu Denis ambaye aliwatoka walinzi wawili wa Azam na kumpasia winga huyo kutoka DR Congo ambaye aliujaza wavuni.
Katika kipindi hicho cha kwanza, Simba ilipata pigo katika dakika ya 21 baada ya beki wake Che Malone Fondoh kuumia ambapo alitolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Chamoue Karaboue.
Matokeo hayo yalidumu hadi refa Ahmed Arajiga kutoka Manyara alipopuliza filimbi ya kuashiria muda wa mapumziko.
Timu zote mbili zilikianza kipindi cha pili taratibu zikionekana kusomana na mpira ulionekana kuchezwa zaidi katikati mwa uwanja.
Ubao wa matokeo ulibadilika dakika ya 76 baada ya Simba kupata bao la pili kupitia kwa Abdulrazack Hamza.
Hamza alifunga bao hilo akimalizia kwa kichwa mpira wa kona uliopigwa na Charles Ahoua.
Wakati ikionekana Simba inaelekea kupata ushindi katika mchezo huo, Zidane Sereri aliyeingia kutokea benchi, aliisawazishia Azam dakika ya 88 akimalizia pasi ndefu ya Feisal Salum maarufu ‘Fei Toto’.
Pamoja na refa wa akiba Hery Sasii kuonyesha dakika tano za nyongeza, hakuna timu iliyoweza kuongeza tena bao.
Matokeo hayo ya sare yameifanya Simba kubakia katika nafasi ya pili ikifikisha pointi 51 huku Azam FC ikifikisha pointi 44.
Yanga inaendelea kuongoza msimamo wa ligi ikiwa na pointi 55.