
Dar es Salaam. Wakati Simba na Azam zikishuka uwanjani jioni ye leo katika Mzizima Derby, vinara na watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga yenyewe leo wamemaliza kazi kwa kuweka rekodi nyingine ya kupata ushindi mkubwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika baada ya kuifyatua Mashujaa kwa mabao 5-0.
Kabla ya kipigo hicho, Mashujaa ilikuwa haijawahi kufungwa idadi kama hiyo tangu ipande daraja msimu uliopita kwenye uwanja wa nyumbani, kwani kipigo kikubwa zaidi mjini humo ilikuwa 3-0 kutoka kwa Azam FC msimu uliopita.
Katika mchezo huo uliopigwa kuanzia saa 10:00 jioni, ilishuhudiwa mabao yote matano yakiwekwa wavuni na nyota wa kigeni, huku mtokea benchi, Clatous Chama akitupia mawili na kumfanya afikishe mabao matatu, wakati Prince Dube alifunga bao la 10 kwa msimu huu akiwa na kikosi hicho.
Ushindi huo wa 18 umeifanya Yanga kufikisha pointi 55 katika mechi 21 na ikiwa haina presha yoyote kwa sasa licha ya wapinzani wao, Simba na Azam zikipepetana kesho usiku, kwani hata zikishinda haziwezi kuing’oa kileleni.
Mashujaa iliyotoka kushinda mabao 2-0 dhidi ya Pamba Jiji baada ya awali kucheza dakika 720 bila kuonja ushindi, ilicheza kwa nidhamu kipindi cha kwanza na kufungwa bao moja tu, kabla ya kipindi cha pili kuelemewa na kasi ya ‘Gusa Achia Pro Max’ ya vijana wa Yanga iliyo chini ya Miloud Hamdi.
MECHI ILIVYOKUWA
Haikuwa kazi ngumu kwa Yanga kwa Yanga kupata ushindi huo kwani ikitawala mchezo huo kwa dakika zote 90, japo kipindi cha kwanza ilipoteza nafasi nyingi ilizotengeneza na kwenda mapumziko ikiwa na bao moja tu lililofungwa na Duke Abuya dakika ya 31 baada ya mabeki wa Mashujaa kujichanganya wakati wa kuokoa mpira langoni mwao na mfungaji kumpiga tobo, kipa Patrick Munthali.
Mashujaa inayofundishwa na kocha Abdallah Mohammed ‘Baresi’ ilijitahidi kuibana Yanga na kufanya isipigwe nyingi katika kipindi hicho cha kwanza.
DUBE KAMA AHOUA, MZIZE
Kipindi cha pili kilianza kwa Yanga kuwashtukiza wenyeji kwa kufunga bao la pili kupitia kichwa cha Prince Dube aliyemalizia krosi tamu ya Pacome Zouzoua aliyeupiga mwingi jana na kuchaguliwa Nyota wa mchezo.
Bao hilo la dakika ya 48 kwa Dube limemfanya afikishe mabao 10 akiungana na Clement Mzize anayekipiga naye Yanga na nyota wa Simba Jean Charles Ahoua wakichuana katika orodha ya wafungaji wa Ligi Kuu kwa sasa ligi ikimalizia raundi ya 21.
PACOME HAFAI
Kiungo Pacome Zouzoua alikuwa moto mbaya kwa Mashujaa akitoa asisti mbili kwa Dube alilofunga kwa kichwa krosi aliyopiga kwa mguu wa kushoto kisha kupiga frikikii iliyounganishwa wavuni na Khalid Aucho likiwa bao lake la kwanza alililoitoa kwa Maxi Nzengeli aliyemuahidi mapema kama angefunga jana angempa Sh 100,000.
Pacome alikuwa akiwachukua na kuwageuka mabeki wa Mashujaa kwa dakika zote 90 alizokuwa uwanjani.
CHAMA DK 9 BAO 2
Kabla ya mchezo huo kulikuwa na maneno mengi juu ya Chama kwamba hana furaha ndani ya Yanga, hivyo akifuta picha akiwa na jezi za timu hiyo lakini jana akaingia dakika ya 69 akichukua nafasi ya Stephanie Aziz KI na kwenda kupiga mabao mawili kwenye dakika za 74 na 82.
Mabao hayo aliyotengenezewa na Duke Abuya na Maxi Nzengeli aliyeingia naye muda huohuo yanamfanya Mzambia huyo fundi kufikisha mabao matatu na asisti mbili tangu asajiliwe na Yanga msimu huu akitokea Simba.
MWENDO WA DOZI
Huu unakuwa ushindi mkubwa wa nne kwa Yanga mkubwa ambapo imezifunga Fountain Gate (5-0), KenGold (6-1) na dhidi ya KMC (6-1) na kuifanya hadi sasa ikiwa imecheza mechi 21 kufikisha mabao 55 sawa na pointi ilizonazo na sasa inaifuata Pamba Jiji iliyoinyoa mabao 4-0 jijini Dar es Salaam.
SINGIDA YABANWA
Katika mechi ya mapema saa 8:00 mchana Singida Black Stars ikiwa nyumbani Uwanja wa Liti, Singida ilibanwa na kutoka sare ya mabao 2-2 na Pamba Jiji, straika Jonathan Sowah akifunga kwa penalti akifikisha bao la nne tangu asajiliwe dirisha dogo, huku Serge Pokou akifunga bao la kwanza akiwa na kikosi hicho, huku mabao ya wageni yakiwekwa na Mkenya Mathew Momanyi aliyefunga mara mbili.