Rais Samia achukua wazo la kuwa ‘kijumbe’ SADC

Dar es Salaam. Katika hali ya utani, Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema wazo lililotolewa na wachekeshaji la kucheza mchezo wa ‘upatu’ linaweza kuwa zuri endapo likibadilishwa na kutafutiwa namna bora ili kusaidia masuala ya kifedha ya nchi za Kiafrika.

Rais Samia amesema wazo hilo likichukuliwa kitofauti litakuwa na mchango wa kujitegemea kifedha, kama wakikubaliana na viongozi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuunda mfuko wao.

Rais Samia ameyasema hayo usiku wa leo Jumamosi usiku Februari 22, 2025 katika hafla ya utoaji tuzo za wachekeshaji Tanzania mwaka 2025.

Mkuu huyo wa nchi amesema kutokana na ufadhili na misaada inayotoka ng’ambo kukatwa mfuko huo unaweza kusaidia maeneo yenye upungufu wa fedha.

Rais Samia alikuwa mgeni rasmi kwenye kilele cha tuzo hizo ambazo zimehudhuliwa watu mbalimbali wakiwemo mawaziri, wasanii na wakuu wa taasisi za umma na binafsi.