
MKUU wa Mkoa (RC) wa Mwanza, Said Mtanda amegeuka kipenzi cha wengi hapa kijiweni kwa vile anafanya kitu ambacho wanakijiwe wamekuwa wakikipendekeza kila siku kwa mabosi wa mikoa.
Kitu hicho ni kutoa sapoti ya kifedha kwa timu za mikoa yao hasa bonasi kwa wachezaji ili kuwahamasisha wafanye vizuri zaidi katika mechi za ligi na mashindano mengine.
Kwa bahati mbaya sapoti hiyo ya fedha imekuwa ikitolewa pindi timu za mikoani zinapocheza mechi dhidi ya timu kubwa za Simba, Yanga au Azam lakini zinapocheza na timu za saizi zao huoni zikiwekewa kibunda mezani.
Sasa hii imekuwa haina faida kwa hizo timu za mikoani kwa vile mechi dhidi ya Yanga, Azam na Simba ni chache hivyo hata ukivuna pointi hapo unaweza usitimize malengo yako kama utapoteza mechi dhidi ya timu za daraja ambalo unalingana nalo.
Hizo mechi kubwa zenyewe unaweza kuziwekea nguvu kubwa na bado ukapoteza ukija kujumlisha na kupoteza dhidi ya timu nyingine za kawaida, ndiyo mwanzo wa timu kushuka daraja na tumeyaona kwa wengi hapo nyuma.
RC Mtanda, Mmwera yule ambaye kapewa jukumu la kuusimamia Mkoa wa Mwanza yeye kaamua kile ambacho kijiweni tunaona ni sahihi kwa kuweka utaratibu wa bonasi kwa kila mechi na Pamba ikipata ushindi inapewa Sh10 milioni.
Hapo hapo Mtanda anatoa kiasi cha Sh250,000 kwa kila bao ambalo Pamba inafunga katika Ligi Kuu na wote si mnaona sasa hivi nyavu zinatikisika tofauti na ilivyokuwa katika mzunguko wa kwanza.
Matunda tunayaona kwa Pamba Jiji kutoka katika kundi la timu mbili zinazoshika mkia, pia kwa sasa haipo hata katika timu mbili zinazoweza kucheza mechi za mchujo kuwania kubaki.
Wakuu wa mikoa yenye timu Ligi Kuu wanapaswa kujifunza kwa mwenzao wa Mwanza, Mtanda, maana anafanya vitu maridadi ambavyo vinaifanya Pamba Jiji kutokuwa na unyonge katika mzunguko huu wa pili, japo juzi ikiwa ugenini dhidi ya Mashujaa ilikumbana na kipigo cha mabao 2-0 mjini Kigoma.