Mgombea CCM, msimamizi wa uchaguzi waungana, wamkana mlalamkaji mahakamani

Kigoma. Mashahidi wawili wa upande wa utetezi katika shauri la uchaguzi wa mwenyekiti wa Mtaa wa Kibirizi, Kata ya Kibirizi, Manispaa ya Kigoma Ujiji, wameungana kumkana mlalamikaji katika shauri hilo, Didas Baoleche kuwa hawamtabui kuwa alikuwa mgombea katika uchaguzi huo.

Mashahidi hao ni aliyetangazwa kuwa mshindi wa nafasi ya mwenyekiti wa Mtaa wa Kibirizi katika Uchaguzi wa Serikali za  Mitaa, Vijiji na Vitongoji wa mwaka 2024, Mrisho Mwamba wa Chama cha Mapinduzi (CCM), na aliyekuwa msimamizi wa uchaguzi huo katika mtaa huo, Gaston Mwanache.

Walikuwa wakitoa ushahidi wao katika shauri hilo lililofunguliwa na Baoleche ambaye alikuwa mgombea katika nafasi hiyo kupitia Chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT- Wazalendo), waliouanza jana na kuhitimisha leo Jumatano, Februari 19, 2025

Mwamba ni mujibu maombi wa kwanza katika shauri hilo na Mwanache ni mjini maombi wa pili na mjibu maombi wa tatu ni msimamizi wa uchaguzi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, ambaye ni Mkurugenzi wa Manispaa.

Licha ya jina lake na chama chake cha ACT- Wazalendo kuonekana katika fomu za matokeo ya uchaguzi alizoziwasilisha mahakamani kama vielelezo vya ushahidi, lakini mashahidi hao wa utetezi walimkana kuwa hakuwa miongoni mwa wagombea.

Hata hivyo, wamepingana kuhusiana na utaratibu wa kutangaza matokeo kama kanuni za uchaguzi huo za Mwaka 2024 zinavyoelekeza.

Kwa mujibu wa kanuni hizo baada ya kura za vituo vyote kujumlisha msimamizi wa uchaguzi Kwa ngazi husika anapaswa kuyatanga akibainisha mshindi na kura alizopata na wagombea wengine kisha anayabandika matokeo hayo.

Mwamba katika ushahidi wake alidai kuwa matokeo hayo yalibandikwa kwanza ndipo yakatangazwa (jambo ambalo ni kinyume na kanuni), lakini Mwanache alidai kuwa alitangaza kwanza matokeo ndipo akayabandika, huku Enita naye alieleza kuwa yalitangazwa kwanza ndipo yakabandikwa.

Katika shauri hilo Baoleche anadai kuwa uchaguzi huo haukuwa huru na wa haki kwa kukiuka kanuni, sheria na taratibu, kwa matokeo kutokutangazwa wala kubandikwa kama⁰ kanuni za uchaguzi zinavyoelekeza na kuingizwa kura bandia ambazo nyingine zilikamatwa.

Anadai kasoro hizo zilisababisha madhara makubwa kwake na wananchi kwa  kunyimwa haki yao ya Kikatiba kumchagua kiongozi wanayemtaka.

Hivyo anaiomba mahakama hiyo itamke kuwa uchaguzi huo ni batili, imuamuru msimamizi msaidizi wa uchaguzi wa mtaa huo atangaze uchaguzi ndani ya siku saba na ndani ya siku 60 uchaguzi mwingine wa nafasi hiyo uendeshwe.

Katika ushahidi wake pamoja shahidi wake mmoja aliyemuita pamoja na mambo mengine, waliieleza Mahakama kuwa kuna mpiga kura mwanachama wa CCM alikamatwa na kura bandia lakini akaokolewa na Polisi ambaye alichukua kura hizo na baadaye akazitumbukiza kwenye sanduku la kura.

Utetezi wa mwamba wa CCM

Mwamba ambaye ni shahidi wa kwanza wa utetezi, kwa mujibu wa ushahidi wake akiongozwa na wakili wake Hamisi Kimilomilo, aliteuliwa kugombea nafasi hiyo na chama chake kisha msimamizi wa uchaguzi.

Siku ya uchaguzi baada ya kupiga kura alirudi nyumbani na akamuacha wakala wake na saa tatu usiku alikwenda ofisi za kata akamkuta matokeo yanabandikwa, baadaye  msimamizi wa uchaguzi alitangaza matokeo  ambapo alimtangaza yeye kuwa mshindi na kuwa mwenyekiti wa Mtaa wa Kibirizi.

Amedai uchaguzi huo ulikuwa huru na wa haki na ameiomba Mahakama ilifutilie mbali pingamizi (shauri) hilo.

Akihojiwa na Wakili wa ACT, Eliutha Kivyiro amejibu kuwa si kweli kwamba Baoleche wa ACT, alikuwa mmoja wa wagombea katika nafasi hiyo.

Hata hivyo amekiri kuwa fomu za matokeo zinaonesha orodha ya wagombea lakini hajaziwasilisha mahakamani kuthibitisha kuwa Baoleche hakuwa mgombea wala fomu ya uthibitisho wa uteuzi wake kuwa mgombea.

Alipoulizwa kama kukosea utaratibu kwa kubandika matokeo na kisha kuyatangaza kama alivyoeleza badala ya kutangaza kwanza kisha kuyabandika amejibu kuwa hilo atajibu msimamizi wa mchaguzi.

Hata hivyo alipoulizwa kwamba kama msimamizi wa uchaguzi atasema tofauti na alivyosema yeye amekubali kuwa yeye (Mwamba), ndio aonekane mwongo, lakini  akaiomba Mahakama ichukue kile alichokisema yeye cha uwongo.

Akihojiwa na wakili wa ACT, Prosper Maghaibuni, amekiri kuwa anamfahamu Ramadhan Kagonga aliyedaiwa kukamatwa na kura bandia, kuwa ni CCM damudamu na kwamba naye siku hiyo alikwenda kupiga kura kituo cha Shule ya Msingi Kibirizi.

Ushahidi wa Mwanache

Mwanache ambaye ni mwalimu na Ofisa Elimu Kata ya Kibirizi ni shahidi wa pili wa utetezi.

Kwa mujibu wa ushahidi wake akiongozwa na Wakili wa Serikali  Fortunatus Mwandu alikuwa msimamizi msaidizi wa uchaguzi na Mtaa wa Kibirizi na ndiye aliyewateua wagombea kutoka vyama sita vikiwemo CCM, Chadema, CUF, TLP, UDP na SAU.

Baada ya kumaliza kujumlisha kura alitangaza matokeo ya washindi kwa wananchi, ambapo alimtangaza mgombea wa CCM kuwa mshindi kwani alipata kura nyingi kuliko wote, kisha kabandika matokeo kwenye ubao wa matangazo.

Amesema kuwa hamtambui Baoleche kama aligombea nafasi hiyo kupitia chama chake kwani alipokea fomu ya utambulisho wake kutoka chama chake na akampatia fomu ya uteuzi ambayo alitakiwa kuijaza na kupata udhamini wa cha kisha airudishe kwa ajili ya uteuzi, lakini hakuirudisha.

“Ndio maana nakiri kwamba sikumteua. Naomba Mahakama tukufu haya madai yatupiliwe mbali kwa gharama,” amesema shahidi.

Akihojiwa na wakili wa ACT Wazalendo, Maghaibuni amekiri kuwa Serikali inafanya kazi kwa nyaraka lakini yeye hakuleta mahakamani nyaraka kuthibitisha kuwa Mwamba aliyemtangaza mshindi, alirejesha fomu ya uteuzi kwake.

Vilevile amekubali kuwa hakuwasilisha ushahidi wa nyaraka hasa fomu za matokeo kuthibitisha kuwa Mwamba alishinda kwa kura nuingi kuliko wengine na kwamba ingawa ni muhimu.

Akihojiwa na Wakili wa ACT Wazalendo, Eliutha Kivyiro kuhusu maelezo ya Mwamba wa CCM aliyemtangaza mshindi, kuwa alibandika kwanza matokeo ndipo akatangaza, Mwanache amesema kuwa hakuwa na uhakika na alichokisema.

Amesema hawezi kukumbuka majina ya wagombea yaliyokuwa kwenye fomu za matokeo isipokuwa la mgombea wa CCM tu, ambaye licha ya kumtanga mshindi kwa kupata kura nyingi, hajui kuwa alipata kura ngapi.

Amekubali kuwa kulikuwa na umuhimu wa kumpinga Baoleche kuwa hakuwa mgombea kwa kuwasilisha orodha ya wagombea (japo hakuiwasilisha).

Licha ya kuwa msimamizi msaidizi wa uchaguzi huo hata hivyo amesema kuwa hajui Sheria (Kanuni) za uendeshaji wa uchaguzi huo.

Shahidi wa tatu, Mwalimu Enita ambaye alikuwa msimamizi wa kituo E Shule ya Msingi Kibirizi amesema hakuna mtu aliyekamatwa na kura Wala vurugu.

Kuhusu wagombea ametaja vyama vilivyoshikiri kuwa ni CCM, UDP, Chadema na AC na vingine havikumbuki.

Amesema hakumbuki mshindi alipata kura ngapi wala mgombea wa ACT hakumbuki kura alizopata.

Pande zote zimefunga ushahidi na Hakimu Kahungu amepanga kutoa hukumu Februari 27, 2025.