Uingereza kuendelea kutoa misaada baada ya Marekani kusitisha

Dar es Salaam. Wakati Serikali ya Marekani chini ya Rais Donald Trump ikikata misaada yake kwa mataifa mengine, Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Marianne Young, amesema nchi yake itaendelea kutoa misaada ya kimaendeleo na kibinadamu kama sehemu muhimu ya ushirikiano wa kimataifa.

Balozi Young amebainisha hayo wakati wa mahojiano maalumu na Mwananchi Jumatatu, Februari 17, 2025, akizungumzia athari za mabadiliko ya sera za kimataifa katika misaada ya kigeni. Ameangazia athari kwa Tanzania na jumuiya ya wafadhili wa kimataifa.

Tangu ameingia madarakani, Januari 20, mwaka huu, Trump alitia saini amri kadhaa za kiutendaji ikiwemo ya kusitisha kwa muda misaada ya kimataifa inayotolewa na shirika la USAID, jambo ambalo limesababisha mamia ya watu kupewa likizo ya bila malipo.

Akizungumzia uamuzi huo wa Marekani, amesema wanatambua Marekani imesitisha utoaji misaada hadi watakapofanya tathmini, hata hivyo amesema Serikali ya Uingereza itaendeleza dhamira yake thabiti ya kutoa misaada ya kimaendeleo na kibinadamu kama sehemu muhimu ya ushirikiano wa kimataifa.

“Tunaamini kwamba hatua shirikishi kati ya washirika wa kimataifa ni muhimu kwa ajili ya kuendeleza viashiria muhimu vya maendeleo, ikiwa ni pamoja na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs),” amesema Balozi Young.

Akizungumzia namna Uingereza inavyosaidia kuziba pengo lililoachwa na Marekani, Balozi Young amesema jumuiya ya wafadhili nchini Tanzania inafuatilia kwa karibu mabadiliko hayo ili kuelewa athari zinazoweza kutokea.

Hata hivyo, amesema kwa upande wa Uingereza, wameongeza kwa kiasi kikubwa bajeti ya Taasisi ya Maendeleo ya Nchi za Nje (ODI) katika mwaka uliopita, kutoka pauni 17 milioni (Sh55 bilioni) hadi zaidi ya pauni 50 milioni (Sh163 bilioni) kwa mwaka 2024–2025.

“Mbali na ufadhili huo, pia tunatumia fedha zinazotolewa na serikali kupitia uwekezaji wa kimataifa wa Uingereza, ambayo imekuwa mdau mkuu nchini Tanzania kwa zaidi ya miaka 50. Kwa sasa, mfumo wetu una pauni 50 milioni (Sh655 bilioni), na tunalenga kuongeza hii maradufu hadi pauni milioni 200 katika miaka michache ijayo.

“Pia, tunazingatia kutumia fedha binafsi. Hili ni eneo muhimu ambapo serikali ya Uingereza inashirikiana kikamilifu na taasisi za kimataifa ili kuongeza msaada wa kifedha na kushughulikia upungufu wa ufadhili uliopo,” amesema.

Balozi Young amezungumzia namna wanavyoshirikiana na Tanzania kusukuma maslahi ya watu wao kama vile sera za kodi, kanuni za uwekezaji na changamoto nyingine, amesema Uingereza inashika nafasi ya pili kwa ukubwa wa uwekezaji kutoka nje ya nchi (FDI) hapa Tanzania.

Amesema Uingereza ina maslahi makubwa katika sekta mbalimbali, ikiwa ni pamoja na nishati, miundombinu na chakula na vinywaji. Amesema wafanyabiashara wa Uingereza hushirikiana mara kwa mara na serikali katika changamoto wanazokutana nazo wanaoingia katika soko la Tanzania.

“Hoja kuu ni pamoja na uwazi na kutabirika, hasa kuhusu madai ya kodi na uchunguzi. Tunafurahi kwamba serikali ilikubali matatizo haya na kuwezesha mijadala iliyosababisha kuanzishwa kwa Tume ya Kodi, ambayo sasa imeanza uchunguzi wake. Tunatazamia kutolewa kwa ripoti ya Tume,” amesema balozi huyo.

Alipoulizwa kama wanaridhishwa na muda unaotumiwa na Serikali kushughulikia changamoto hizo, Young amesema, kwa kutumia mfano wa kodi, serikali ilikubali haraka wasiwasi wao na kuomba mifano mahususi, ambayo walitoa mara moja pamoja na vithibitisho na takwimu zinazoshabihiana.

“Katika kujibu, serikali iliwaita haraka makamishna kuchunguza masuala hayo. Sasa tuna matumaini kwamba mapendekezo yatawasilishwa hivi karibuni na kwamba hatua madhubuti itafuata mara moja,” amesema Balozi Young.