Sauti za Busara 2025 ilivyotumika kupigania amani ya dunia

Zanzibar. Tamasha la Muziki la Sauti za Busara la 22, lililoanza Februari 14, 2025 limetamatika usiku wa kuamkia leo Jumatatu Februari 17, 2025 kwa burudani ya kusisimua kutoka kwa wasanii wa ndani na nje ya nchi Tanzania kama vile Zenji Boy, Blinky Bill, Thandiswa na wengineo.

Tamasha hilo la siku tatu (sawa na saa 72) lililofanyikia

Ngome Kongwe, Stone Town kisiwani Unguja, Zanzibar kwa mwaka huu lililenga kupaza sauti kwa ajili ya kuleta amani duniani kupitia muziki, limefanikiwa kuzileta pamoja sauti za wasanii kutoka mataifa mbalimbali.

Ujumbe huo unakuja wakati dunia na Afrika ikishuhudia machafuko katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia Congo ambako waasi wa M23 wanaendeleza mapigano, huku wakitwaa baadhi ya miji ya nchi hiyo.

Kaulimbiu hiyo ya tamasha hilo la kimataifa ilitolewa Februari 14,2025 na Mtendaji Mkuu wa tamasha hilo, Journey Ramadhan wakati akifanya ufunguzi wake.

Mtendaji Mkuu wa Sauti za Busara, Journey akisisitiza wadau wa muziki kuhusu amani

“Nina ujumbe mdogo kuhusu kwanini tuliamua kuchagua kaulimbiu hii kwa mwaka huu. Katika dunia ambayo migogoro inatisha. Kila mmoja wetu ana nguvu ya kuwa sauti ya amani.

“Tumeshuhudia migogoro mingi Afrika, kama ninavyosema. Tuache muziki uzungumze kwa sababu sauti za amani zinanza leo hadi tarehe 16 Februari,” alisema Journey wakati akifungua tamasha.

Naye Zakia Lulu ambaye ni Meneja Masoko wa Sauti za Busara amesema furaha yake kubwa katika tamasha la 2025 ni kuona watu wote wameungana wakitaka amani.

“Kila bendi jukwaani inatumbuiza, na kila wakati wanaposema ‘Voices for Peace’ au wanapozungumzia jambo lolote linalohusiana na amani. Ninyi nyote mnaungana. Yaani, naona tuko pamoja kwenye kutaka amani. Furaha yangu tumeungana na kukubali kupaza sauti kwa ajili ya amani,” alisema Zakia

Katika mandhari ya kuvutia ya Zanzibar, baadhi ya wasanii kama Frida Amani, Ukhoikhoi walitumbuiza siku ya kwanza ya tamasha hilo.

Aidha, siku ya pili ya tamasha lilifunguliwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Sauti za Busara, Simai Mohammed Said, kwa wimbo  uitwao Afrika ulioimbwa na Salif Keita (Mali). Ukiwa umebeba maudhui ya upendo, umoja, na kujivunia urithi wa bara la Afrika.

Haikuishia hapo baadhi ya wasanii waliopanda jukwaani kwa siku hiyo ni Baba Khas (Tanzania), Ukhoikhoi (Afrika Kusini), Mumba Yachi (Congo). Ambapo naye Christian Bella aliifunga siku hiyo kwa kuwapa vibe mashabiki kwa kutumbuiza ngoma zake kama vile ‘Nani kama Mama’, Subira na nyinginezo.

Mbali na siku hizo zote mbili ambazo mashabiki walijaza uwanja na kucheza kwa furaha. Tamasha hilo lilitamatishwa kwa sauti za wakali  kutoka mataifa mbalimbali kama Zenji Boy, Blinky Bill (Kenya) na kufungwa na msanii wa Afrika Kusini Thandiswa. 

Hivyo, basi jukwaa la Sauti za Busara lilipambwa na wakali kama vile Thandiswa (Afrika Kusini), Blinky Bill (Kenya), Christian Bella & Malaika Band (Tanzania). Bokani Dyer (Afrika Kusini), The Zawose Queens (TZ/UK).

Kasiva Mutua (Kenya), Zanzibar Taarab Heritage Ensemble (Zanzibar), Leo Mkanyia & Swahili Blues (Tanzania), Boukouru (Rwanda), Tryphon Evarist (Zanzibar), Charles Obina (Uganda), Baba Kash (Tanzania).

Frida Amani (Tanzania), Assa Matusse (Msumbiji), Mumba Yachi (Congo), Nidhal Yahyaoui (Tunisia), Étinsel Maloya (Reunion), WD Abo (Sudan), B.Junior (Mayotte), uKhoiKhoi (Afrika Kusini), na Joyce Babatunde (Kamerun)

Walichosema wasanii

Akizungumza na Mwananchi, mwanamuziki wa singeli, Baba Kash amesema ni mara yake ya kwanza kupanda kwenye jukwaa hilo, lakini mapokeo ya mashabiki yalikuwa makubwa tofauti na alivyotegemea.

“Mimi mwanzoni nilikuwa naimba na Dj, lakini nikaona hapana. Nikaanza kutengeneza ladha ya Singeli, Mchiriku na Mnanda kwa pamoja nikiwa napiga bendi. Nimefanikiwa katika hilo ndiyo maana nimepata nafasi ya kutumbuiza Sauti za Busara 2025. Hii ni mara ya kwanza, lakini imekuwa poa sana,” amesema.

Naye msanii wa Congo Christian Bella amesema ni zaidi ya mara mbili anashiriki.