
Dar/Mikoani. Ni kilio kila kona, wananchi wakilalamikia tozo ya huduma ya choo inayokusanywa kwenye stendi kuu za mabasi za mikoa nchini.
Ufuatiliaji uliofanywa na Mwananchi umebaini licha ya wananchi kuridhia malipo ya tozo ya kati ya Sh200 hadi Sh300 kwa huduma kwenye vyoo vya stendi, wanalalamikia tozo zingine wanazotozwa ili kuingia ndani ya maeneo hayo.
Pia wanahoji sababu za kuendelea kutozwa wakati huduma sawa na hizo hutolewa bila malipo maeneo mengine ya usafiri kama bandarini, stesheni za treni na viwanja vya ndege.
Katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, malalamiko yapo kuhusu tozo hiyo kwenye stendi za mabasi Nyegezi, Nyamhongolo, Tabora na Bariadi, licha ya kulipia Sh200 ili kuingia stendi.
Si hivyo, wanalalamika licha ya kulipia huduma ya vyoo, baadhi ni vichafu, havina huduma ya maji wala sabuni na hivyo kuhoji ni nini matumizi ya fedha zinazokusanywa.
Sabatho Jonhson, abiria aliyekutwa stendi ya mabasi Nyamhongolo, wilayani Ilemela, Mwanza alisema licha ya kutozwa Sh200 ili kuingia ndani ya stendi pasipo kujali alikuwa na tiketi mkononi, bado alitozwa Sh200 kwa ajili ya huduma ya choo.
Mkazi wa Musoma, mkoani Mara, Benadeta Mafuru alisema abiria ni wateja kama walivyo wengine, wanapaswa kuhudumiwa bure, akitoa mfano wa abiria wanaosafiri na meli, ndege na treni, ambao hawatozwi kwa huduma za vyoo.
Mfanyabiashara wa dagaa kati ya Mwanza na Dodoma, Joyce Andrew alisema ni jambo la ajabu stendi binafsi za mabasi hazitozi huduma za vyoo, lakini za Serikali zinazosimamiwa na halmashauri hutoza.
Wile Aron, mkazi wa Maswa alisema licha ya huduma ya choo katika kituo cha mabasi cha mjini Bariadi kuwa nzuri kutokana na usafi, maji ya kutosha na sabuni, lakini ilipaswa kuwa bure.
Ramadhani Jumanne, wakala wa kampuni moja ya mabasi yenye ofisi ndani ya stendi hiyo ya Bariadi, alisema si abiria pekee wanaotozwa Sh300 kwa huduma za vyoo licha ya kulipia kuingia stendi, hata wao kwa mwaka wanalipa Sh56, 000 za tozo ya huduma lakini wanapoingia kituoni hapo asubuhi wanalipia Sh500 ambazo ni nje ya huduma za kijamii, ikiwemo ya choo.
“Hapa tunalipia kwa mwaka lakini kila siku lazima tulipie Sh500 ndipo tuingie stendi na ukienda chooni unalipia Sh300, inatuumiza kwa kuwa usipojizuia unaweza kutumia hadi Sh1, 500 kwa huduma ya choo pekee kwa siku,” alisema.
Alisema gharama zote zinalipwa lakini usafi pia haufanyiki vizuri na kwa wakati, matundu ya vyoo ni machache kwa wanaume yakiwa matatu na kwa wanawake matatu, hali inayosababisha foleni hasa wakati wa asubuhi na mchana mabasi mengi yanapoingia kituoni.
Sadala Kulwa, mkazi wa Manispaa ya Tabora pia alisema hali ya usafi hairidhishi na hivyo wapo baadhi ya watu ambao hujisaidia haja ndogo kwenye chupa.
“Mifumo ya ushuru isipowekwa vizuri tatizo la watu kujisaidia kwenye chupa haliwezi kuisha kwa kuwa mtu hawezi kutumia kati ya Sh1, 000 hadi Sh1,500 kwa siku kwa ajili ya choo pekee, haiwekani,” alisema.
Mkoani Dar es Salaam
Katika kituo cha mabasi cha Magufuli, Malik Sefu mkazi wa Tegeta alisema haoni sababu ya watu kulipia gharama ya choo kwa sababu ni huduma muhimu ambayo kila binadamu anapaswa kuipata bila kujali uwezo wake wa kifedha.
“Hicho kiasi (Sh300) kinaweza kuonekana kidogo lakini nina uhakika kuna watu wanashindwa kumudu, halafu kwa nini vyoo vya stendi tu ndiyo tunalipia, mbona vya vituo vya treni au uwanja wa ndege hatulipii hizi huduma,” alihoji.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha Shirika la Reli Tanzania (TRC), Fred Mwanjala alisema hakuna gharama inayotozwa kwa abiria na wasindikizaji wanapohitaji kutumia huduma za vyoo.
“Vyoo ni bure kwa watu wote kwa sababu hiyo ni huduma muhimu, kwenye suala la utunzaji na usafi wa vyoo hivyo shirika limetoa tenda kwa kampuni ambayo ndiyo inafanya kazi hiyo chini ya usimamizi wa TRC kuhakikisha viko safi na salama muda wote,” alisema.
Hali Dodoma, Mbeya
Katika stendi ya mabasi yanayokwenda mikoani Nanenane jijini Dodoma abiria au msindikizaji hutakiwa kulipia ushuru wa Sh300 getini na Sh300 kwa huduma ya vyoo.
Magreth Chibago, wakala wa mabasi kwenye stendi hiyo alisema ni kero ya muda mrefu lakini kila wakipaza sauti hakuna anayewasikiliza.
Alisema kutokana na gharama hizo, baadhi ya watu wamekuwa wakijisaidia kwenye chupa na vikopo, kisha kuvitelekeza stendi, hali inayohatarisha afya za watu wengine.
Michael Masoud, alishauri kodi ikusanywe pamoja, akisema, “unakuta mwingine anasafiri na familia yake, wakiwemo watoto ambao hawawezi kujizuia wakibanwa na haja, wakitaka huduma ya choo wanatakiwa kulipia kwa kila mtu, hizi gharama ni kubwa ni vyema ikatolewa bure,” alisema.
Licha ya huduma nzuri kutolewa jijini Mbeya, Yusuph Bena ameuomba uongozi wa halmashauri kuangalia upya gharama za kuingia stendi kuu sambamba na huduma za vyoo, ambazo ametaka ziunganishwe.
“Mtu kuingia stendi kuu ni Sh200, gharama ya choo Sh200 hadi Sh300 sasa mfumo ungesoma kitu kimoja halafu mwananchi akaondokana na usumbufu wa kuwa na tiketi zaidi ya moja kwenye eneo moja,” alisema.
Mmoja wa watoa huduma ya tiketi katika stendi hiyo upande wa vyoo, alisema wanatozwa mara mbili kutokana na uwepo wa wazabuni wawili tofauti, japokuwa mfumo ni mmoja.
“Kila eneo lina gharama zake kwa kuwa wazabuni ni wawili na wanatofautiana ila mfumo ni mmoja, kwa hiyo hatuwezi kuzungumzia zaidi lakini wananchi wanajua,” alisema.
Maoni ya wadau
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shirika la Kutetea Haki za Abiria nchini (Shikuha) Februari 7, 2025 na kuthibitishwa na Katibu Mkuu wake, Hashim Omary, ilisema vyoo vya stendi vina gharama za uendeshaji lakini ni muhimu kutathmini iwapo ushuru wa stendi unaokusanywa kutoka kwenye mabasi haupaswi kugharamia huduma hizo, badala ya kuongeza mzigo kwa abiria.
Shirika hilo lilisema kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa ya mwaka 1982 na kanuni zake, halmashauri zina mamlaka ya kutoza ushuru wa huduma kwa mabasi yanayoingia kwenye stendi, ushuru unaotumika kwa uendeshaji wa miundombinu ya stendi, ikiwa ni pamoja na usafi wa mazingira, usalama na huduma za msingi kama vyoo.
“Kwa kuwa ushuru huu unatozwa kwa kila basi linalotumia stendi, inapaswa kuwa sehemu ya bajeti ya halmashauri kuhakikisha vyoo vinasafishwa na abiria wanatumia huduma hiyo bila malipo ya ziada.
Alisema kutoza ushuru kwa mabasi halafu pia kuwatoza abiria kwa matumizi ya vyoo ni aina ya utozaji kodi mara mbili, inayokiuka misingi ya haki kwa abiria na kuongeza gharama zisizo na msingi kwao.
“Kifungu cha 16 cha Sheria ya Ushuru wa Huduma kinataka makusanyo yote ya ushuru wa huduma kutumika kwa kuboresha mazingira ya biashara na utoaji wa huduma bora kwa wananchi. Hii inamaanisha kuwa, sehemu ya ushuru wa stendi inatakiwa kutumika kwa usafi wa vyoo badala ya kuwatoza tena abiria,” limesema shirika hilo.
Shirika hilo limezitaka halmashauri kuhakikisha ushuru unaokusanywa kwa mabasi unatumiwa ipasavyo ili kuondoa mzigo kwa wananchi na kuleta uwazi katika matumizi ya mapato ya umma, kwa kuwa hilo si suala la biashara tu, bali ni haki ya msingi ya abiria kupata huduma bora bila kutozwa gharama za ziada.
Mkufunzi wa Vitendo Chuo cha SAUT mkoani Mwanza, Martin Nyoni alishauri mamlaka kubadili mfumo wa biashara ya vyoo katika vituo vya mabasi akieleza kinachofanyika ni kama mwananchi analipa tozo juu ya tozo.
Naye, Mtaalamu wa uchumi, Inocent Fidelis alisema huduma hiyo ni ya msingi inapaswa kutolewa bure na iwapo kuna gharama za uendeshaji ni vizuri kuwe na vyanzo vingine kwa ajili ya kuiendesha.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Adrian Jungu alisema madiwani kupitia baraza lao waliweka sheria ndogo za kituo hicho cha mabasi ambayo inaelekeza katazo na adhabu kwa wanaokiuka kulipia huduma ya choo na ushuru wa kiingilio getini.
“Sheria ambayo ilipitishwa inaelekeza matumizi ya vyoo kwenye kituo cha mabasi mjini Bariadi italipiwa kwa viwango vilivyoainishwa, ni kosa kwa mtu yeyote kuingia katika kituo chetu cha mabasi pasipo kulipia ushuru husika,” alisema.
Alisema atakayekiuka masharti ya sheria ndogo hizi, atakuwa ametenda kosa na iwapo atapatikana atatozwa papo hapo faini isiyopungua Sh50, 000 na akishindwa atafikishwa mahakamani.
Alisema walijenga kituo hicho ikiwa ni sehemu ya chanzo cha mapato ya ndani ili waweze kutekeleza mipango waliojiwekea kwa ajili ya kuwaletea maendeleo wananchi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Elias Kayandabila alisema fedha zote zinazotozwa katika kituo cha mabasi ni kwa mujibu wa sheria ndogo ndogo za halmashauri, hivyo kama wananchi wameona kwao ni changamoto wafuate utaratibu wa kupeleka maoni yao yafanyiwe kazi.
“Ni sheria kutoza hivyo, lakini kama wananchi wanaona shida wafikishe maoni kwa viongozi katika maeneo yao akiwemo diwani wa eneo husika ili yapitishwe kwenye vikao vya maendeleo ya kata, halafu wao walete ngazi ya halmashauri yajadiliwe kwenye Baraza la Madiwani na hatimaye utaratibu usimamiwe,” alisema.
Imeandikwa na Saada Amir, Hawa Kimwaga, Samwel Mwanga, Saddam Sadick, Rachel Chibwete na Elizabeth Edward.