
ACHANA na rekodi ya kuburuza mkia katika Ligi Kuu Bara tangu ilipoanza, sare ya bao 1-1 iliyoipata KenGold dhidi ya Tabora United juzi imeifanya kuandika rekodi ya kupata pointi kwa mara ya kwanza msimu huu ugenini, kwani kabla ya hapo ilikuwa haijashinda wala kutoka sare yoyote.
Katika mchezo huo ambao KenGold ilitangulia kupata bao la penalti kupitia kwa Selemani Bwenzi dakika ya 25, kisha Heritier Makambo akaisawazishia Tabora United dakika ya 87 umeifanya kuvuna pointi moja ugenini kwa mara ya kwanza.
Kikosi hicho kilichopanda Ligi Kuu Bara msimu huu, mchezo wake na Tabora United ulikuwa wa 11 kucheza ugenini ambapo kati ya hiyo kimetoka sare mmoja na kupoteza 10 na kwa ujumla kimefunga mabao matano na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 25.
KenGold ilianza msimu huu na Kocha Fikirini Elias aliyeiongoza katika michezo mitatu ikichapwa yote kisha Septemba 17, mwaka jana akajiweka pembeni mwenyewe kwa kile alichoeleza kuwa ni kufikia makubaliano ya pande mbili.
Baada ya hapo ikaongozwa na Jumanne Challe aliyeipandisha Ligi Kuu Bara kama kocha wa muda kutokana na kutokidhi vigezo vya kusimamia benchi la ufundi, ambapo alisimamia michezo mitano akishinda mmoja, sare mmoja na kupoteza mitatu.
Oktoba 22, 2024, uongozi wa KenGold ulimtangaza Omary Kapilima kuiongoza ambapo hadi sasa ameisimamia katika michezo 11 ya Ligi Kuu Bara na kati ya hiyo ameshinda mmoja, sare mitatu na kuchapwa saba.
KOCHA HUYU HAPA
Akizungumzia kiwango cha timu hiyo, Kapilima alisema kitendo cha kupata pointi nne katika michezo miwili iliyopita sio jambo baya, kwani kabla ya hapo walikuwa hawana mwenendo mzuri ambao umewafanya kushika nafasi waliyopo.
“Kadri tunavyoendelea kupata pointi zinazidi kuongeza morali ya wachezaji kwa sababu ukiangalia tulipo bado sio sehemu salama sana. Tunaendelea kufanyia kazi changamoto zilizopo ikiwemo namna ya kucheza kwa nidhamu katika kila mchezo,” alisema.
Kapilima ameendelea kuiongoza timu hiyo licha ya Januari 18, mwaka huu, uongozi kumtangaza Kocha Vladislav Heric, raia wa Serbia, ambaye hadi sasa bado hajapata vibali vya kufanya kazi hapa nchini.
Heric aliyezaliwa Agosti 29, 1966 amezifundisha Club Africain ya Tunisia, Maritzburg United, Polokwane City, Cape Town na Chippa United za Afrika Kusini, huku akikabiliwa na kazi kubwa ya kukinusuru kikosi hicho kisishuke daraja.
Kocha huyo aliwahi kucheza soka akianza 1976 akiwa na FK Vojvodina’s akademi kisha soka la kulipwa FK Proleter Novi Sad na FK Fruskogorac Novi Sad. Ana leseni A ya UEFA.
Heric ambaye ni mzoefu soka aliacha kucheza soka la ushindani akiwa na umri wa miaka 21 baada ya kuandamwa na majeraha ya mara kwa mara, jambo lililomfanya kujikita kusomea ukocha kufuatia ndoto zake kufifia mapema.