Hamas yawaachilia mateka watatu wa Israel, Wapalestina 369 kunufaika

Gaza. Kundi la Hamas limewaachilia huru mateka watatu wa Israel waliokuwa wakishikiliwa katika eneo la Gaza, huku Israel ikitarajiwa kuwaachia Wapalestina 369 waliokuwa wakitumikia vifungo.

Utaratibu wa kuachia mateka ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofanyika kuanzia Januari 2025 kati ya Hamas na Jeshi la Israel (IDF).

Mateka waliokombolewa ni Sagui Dekel-Chen (Mmarekani mwenye asili ya Israel), Alexander Sasha Trufanov (raia wa Russia mwenye asili ya Israel), na Yair Horn (raia wa Italia mwenye asili ya Israel).

Walikabidhiwa kwa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu, na baadaye kurudishwa Israel kwa uchunguzi wa kitabibu na kuungana na familia zao.

Wote watatu walikuwa miongoni mwa waliotekwa na Hamas kufuatia shambulio lake la Oktoba 7 kusini mwa Israel.

Dekel-Chen, Trufanov na Horn walionekana wakibeba vyeti vya kuachiliwa kwao na ramani za Palestina. Walirudishwa Israel kwa uchunguzi wa kitabibu kabla ya kuunganishwa na familia zao.

Kuachiliwa kwao leo Februari 15, 2025 kumefanya idadi ya mateka waliotolewa na Hamas na Jihad ya Kiislamu ya Kipalestina imefikia 25 tangu mpango wa usitishaji mapigano ulipoanza Januari 19, 2025.

Mamia ya raia wa Kipalestina, wakiwemo wanawake, watoto na wazee, walikusanyika nyuma ya kizuizi cha usalama kushuhudia tukio hilo.

Mwandishi wa Al Jazeera, Tarek Abu Azzoum, akiripoti kutoka Khan Younis, alieleza maandalizi ya tukio hilo kuwa yanaonekana kupangiliwa kwa uangalifu na yenye kuzingatia itifaki kali ya usalama na onyesho la nguvu la kimamlaka.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya eneo la Gaza, mapigano hayo yaliyoanza Oktoba 7,2023, yamesababisha vifo vya Wapalestina zaidi ya 47,000 huku zaidi ya 111,000 wakijeruhiwa huku Waisrael zaidi ya 1,200 wakiuawa na wengine zaidi ya 200 kuchukuliwa mateka.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.