
WAKATI Ofisa Habari wa klabu ya Simba, Ahmed Ally akitamba kwamba straika wa timu hiyo, Leonel Ateba amechora tattoo ya Mnyama Simba kutokana na mahaba aliyonayo kwa klabu hiyo, nyota huyo kutoka Cameroon amevunja ukimya na kuanika maana halisi ya mchoro huo.
Ateba amechora mchoro huo katika bega la kushoto, na kuzua maswali mengi kabla ya Ofisa Habari huyo kutoa ufafanuzi huo, akidai amefanya hivyo kuonyesha mahaba aliyonayo kwa klabu hiyo ya Msimbazi aliyojiunga nayo msimu huu akitokea USM Alger ya Algeria.
Hata hivyo, mshambuliaji huyo mwenye mabao manane katika Ligi Kuu Bara kwa sasa akiwa sambamba na nyota mwenzake wa Simba, Jean Charles Ahoua, amefafanua ukweli kuhusu mchoro huo alipozungumza na Mwanaspoti.
Ateba, amesema kilichomsukuma kuchora mchoro huo ni mnyama Simba ni mbili na amefanya kwa upendo wa dhati na sio kulazimishwa.
Ametaja sababu ya kwanza ni timu ya taifa lake inaitwa Indomitable Lions (Simba wasiofungika) waliobeba ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) mara tano AFCON, lakini jingine ni klabu yake ya sasa ya Simba, hivyo akaamua kuchora tattoo hiyo kama ishara ya kuonyesha upendo wake wa kufurahi kuzitumikia.
“Ni timu ninazozipenda ndio maana nimeona kitu pekee kitakachoonyesha upendo ni kuchora tattoo, ambayo inawakilisha klabu ninayoitumikia na timu yangu ya taifa y Cameroon ambao nao wanaitwa Simba, lakini ni wale wasiofungika,” amesema Ateba ambaye msimu uliopita akiwa na USM Alger alifunga bao moja katika mechi 12.
Nyota huyo mwili jumba, amesema ameona namna ambavyo mashabiki wa Simba walivyolipokea tattoo yake kwa upendo, huku wengine wakimposti katika mitandao yao ya kijamii, jambo linalomuongezea nguvu ya kupambana zaidi, ili mchango wake wa kupigania ubingwa kwa msimu huu uwe mkubwa.
“Najisikia faraja na naamini nitakuwa nimewajibu vyema watu ambao walikuwa wanajiuliza kuhusiana na jambo hilo,” amesema Ateba ambaye akishirikiana na nyota wenzake wameiwezesha Simba kurudi kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu kwa kufikisha pointi 47, moja zaidi na ilizonazo Yanga.