
Dar es Salaam. Uamuzi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kilimanjaro kumfuta uanachama kada wake, Dk Godfrey Malisa umechukua sura mpya baada ya kada huyo kusema hatambui kilichofanyika.
Makisa anayejiita kada mwandamizi wa CCM, amesema mpango wake wa kwenda mahakamani kupinga uamuzi wa Mkutano Mkuu wa CCM kumpitisha Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea wa nafasi hiyo, bado upo pale pale na anaendelea na mchakato.
Dk Malisa ametangaza uamuzi huo mpya leo Februari 11,2025 alipozungumza na Mwananchi juu ya hatua zilizochukuliwa kwake jana na Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Mercy Mollel aliyetangaza kuvuliwa uanachama wa CCM wa kada huyo.
Mollel akizungumza mbele ya wandishi wa habari jana Jumatatu Februari 11, 2025 mjini Moshi alisema; “tulikuwa na kikao cha Halmashauri kuu ya CCM Mkoa wa Kilimanjaro ambacho pamoja na mambo mengine kimemfukuza mwanachama wa CCM Dk Godfrey Malisa kwa sababu amekuwa akibeza uamuzi uliofanyika na Mkutano Mkuu CCM Dodoma Januari 19, 2025. Baada ya mkutano ule, Dk Malisa amekuwa akitoa matamko ambayo hayaleti umoja na mshikamano ndani ya chama na katika nchi yetu.”
Kifungu kilichotumika kumfukuza uanachama Dk Malisa, katibu huyo amekinukuu kuwa ni cha tatu(c) cha Katiba ya CCM.
Akitangaza uamuzi huo, Katibu Mollel amenukuu kifungu hicho kinasema; ‘Mwanachama yeyote atakayekataa kumuunga mkono mgombea wa CCM aliyeteuliwa na kikao halali cha chama na kuthubutu kufanya kampeni za siri au wazi kumhujumu, atakuwa ametenda kosa la usaliti na adhabu ni kufukuzwa uanachama.’
Uamuzi huo unapingwa na Dk Malisa ambaye ameiambia Mwananchi kwamba hakushirikishwa na hakupewa barua yoyote ya kufukuzwa uanachama.
Lakini Mwananchi limemrejea Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Mollel ili azungumzie madai ya Dk Malisa kuwa yatajibiwa na Diwani wa Kata ya Miembeni na Katibu Mwenezi mstaafu wa CCM Wilaya ya Moshi Mjini, Mohamed Mushi.
Mwananchi limebisha hodi kwa Mushi ili kupata undani wa sakata hili na akijibu kwa simu, amesema walimshirikisha Dk Malisa hatua anazochuliwa na aliitwa kujieleza kuanzia ngazi ya tawi hadi kata.
“Tulimtumia wito wa kuhudhuria kikao cha kamati ya maadili ya tawi Januari 26 na Januari 28, 2025, kun wazee wa chama tuliwatuma mpaka nyumbani kwake akasema atakuja na Januari 31,2025 alifika na kusomewa tuhuma zake na kutakiwa kujibu na alikiri video ile ni yake.
“Alipewa nafasi ya kusikilizwa ngazi ya tawi kwa kamati ya maadili ya tawi lakini hakuwa tayari kuzungumza, tukachukua hatua, maamuzi yakaenda hadi juu akafukuzwa uanachama, wenye mamlaka ya chama ni viongozi wa chama, jambo linaloamuliwa na kikao taarifa inaweza kutoka kwa barua au kwa mdomo,”amesema.
Kauli ya Malisa
Akizungumza na Mwananchi leo Februari 11, 2025 kwa simu, Dk Malisa amekiri kuitwa na CCM kata na aliandikiwa barua na alifika kwenye mkutano lakini aliomba kutozungumza.
Amesema hoja yake ni kikao kilichoketi cha CCM mkoa kumuondoa uanachama bila kumshirikisha wala kumpa barua ya kumfukuza uanachama.
Kutokana na hayo, amesema hawezi kupinga uamuzi uliotolewa jana, kwa sbbu hana barua na taarifa amezipata kupitia vyombo vya habari.
“Ukisema niende mahakamani kupinga, nitapinga nini, taarifa za kufukuzwa uanachama nimezisikia tu sikupata barua yoyote, na sijui kama chama changu kinautararifu wa kufukuza wanachama wake kupitia taarif kwa vyombo vya habari,” amesema Dk Malisa.
Kuhusu hatua yake ya kuendelea kupinga uamuzi wa Mkutano Mkuu wa CCM, Dk Malisa amesema mpango wake uko pale pale na taratibu zinaendelea.
Atakayeshitakiwa katika kesi ile, Dk Malisa amesema ni bodi ya wadhamini ya CCM na mpaka sasa wanaendelea kukamilisha michakato ya kisheria.
Amesema dhumuni la kesi ni kupinga kitendo cha CCM kumpitisha mgombea mmoja wa nafasi ya urais bila kutoa fursa kwa wanachama wengine.
Amesema huko mahakamani ndiko kutatambulika kama amefukuzwa kwani kukiwa na hoja hiyo ataiomba mahakama apewe barua ya kufukuzwa uanachama na ataupinga ila sasa bado ni mwanachama na hana taarifa za kufukuzwa.
Dk Malisa amesema kuna utaratibu wa wazi wa wagombea wa nafasi ya urais wanavyotapatikana huku akisistiza utaratibu uliofanyika hivi karibuni wa kumpitisha Rais Samia kugombea nafasi hiyo haukuwahi kushuhudiwa ndani ya CCM.
Azimio la Rais Samia kuwa mgombea kwenye nafasi ya urais limepitishwa na Mkutano Mkuu wa CCM ambao ndiyo chombo cha mwisho cha uteuzi wa mgombea wa tiketi ya urais kupitia chama hicho.
Mbali na Rais Samia, wengine waliopitishwa kwenye kinyang’anyiro hicho cha kiti cha U – rais, ni Dk Hussein Mwinyi kwa upande wa visiwani.
Uamuzi wa mkutano mkuu wa CCM umefanyika mapema kuliko kawaida, na katika mkutano ambao awali haukupangwa kufanya maamuzi hayo katika ajenda zake.
Inaelezwa katika mkutano huo uliopitisha jina la Rais Samia kulikuwa na ajenda kuu moja ya kupitisha jina la Makamu wa Mwenyekiti (Bara) ambapo mwanasiasa mkongwe Stephen Wasira akipitishwa kushika wadhifa huo jana Jumamosi.