
Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepanga Februari 26, 2025, kuwasomea hoja za awali (PH) Sophia Mwenda (64) na mwanaye, Alphonce Magombola(36) wanaokabiliwa na kesi ya mauaji.
Mwenda ambaye ni mkazi wa Mbagala anadaiwa kushirikiana na mtoto wake huyo wa kiume, kumuua Beatrice Magombola, ambaye ni binti yake wa kumzaa mwenyewe.
Uamuzi huo umetolewa leo Jumanne, Februari 11, 2025 na Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kusomewa maelezo mashahidi.
Hata hivyo, kesi hiyo baada ya kusome PH, itaanza kusikilizwa katika Mahakama hiyo, baada ya Hakimu anayesikiliza kesi hiyo kuongezewa Mamlaka ya nyongeza kusikiliza kesi za mauaji.
Hakimu Lyamuya amepanga tarehe hiyo, baada ya wakili wa Serikali, Asiat Mzamiru kuoimba Mahakama hiyo ipange tarehe kwa ajili ya Serikali kuwasomea washtakiwa maelezo yao.
Mzamiru amedai kesi hiyo ilipagwa kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo yao, lakini hakimu anayesikiliza kesi hiyo, Franco Kiswaga hayupo hivyo wanaomba mahakama ipange tarehe nyingine.
Lyamuya amekubaliana na ombi la upande wa mashtaka na kuahirisha kesi hiyo hadi Februari 26, 2025.
Washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na kesi ya mauaji kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.
Kwa mara ya kwanza washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo, Julai 15, 2022 na kusomewa kesi ya mauaji namba 3 ya mwaka 2022.
Katika kesi ya msingi, washtakiwa Washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa la mauaji Desemba Mosi, 2020, eneo la Kijichi, Wilaya ya Temeke.
Inadaiwa siku hiyo, majira ya usiku, Mwenda na Alphonce wanadaiwa kumuua Beatrice Magombola, ambaye ni mwana familia na kinyume cha sheria.
Washtakiwa baada ya kusomewa shtaka linalowakabili siku hiyo, hawakurusiwa kujibu chochote kwa sababu Mahakamani hiyo, haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji.