ELIMU & MAADILI: Ningefundisha hivi maadili darasa la tatu, nne

Ni jambo jema kwamba tumeanza mtalaa mpya shuleni ambao una somo la maadili likifundishwa pamoja na somo la historia ya Tanzania.

Hivi karibuni nimeandika makala katika gazeti hili, nikapendekeza kwamba somo la maadili lisimame lenyewe na lisifundishwe pamoja na somo lingine kama ilivyo sasa.

Ikumbukwe kwamba somo la maadili ni somo mama kwa masomo yote, kama vile uadilifu ni tabia mama katika utu wetu.

Kulipanga somo hili pamoja na somo lingine ni kukosa kuelewa uzito wake na umuhimu wake katika mfumo wote wa elimu.

Hata hivyo, ni vema kwamba walau somo hili lipo darasani sasa, hata kama linafundishwa pamoja na somo lingine. Ni mwanzo mzuri.

Katika kitabu cha darasa la tatu cha Historia ya Tanzania na Maadili, nimeona kwamba nafasi iliyotengwa kwa somo la maadili ni ndogo. Maana ya neno “maadili” haielezwi kwa kinagaubaga.

Nimeshuhudia mjukuu wangu wa darasa la tatu akihaha kuelewa maana ya neno maadili. Mifano inayotolewa kuhusu maana ya maadili haitoshi na lugha inayotumika si rafiki kwa watoto wa umri huu.

Tufundishe vipi maadili?

Napendekeza tuboreshe mwonekana wa somo hili katika mtalaa uliopo. Mimi ningekuwa mwalimu wa somo la maadili darasa la tatu na la nne, ningeanza kama ifuatavyo. Ningewapanga wanafunzi katika makundi ya wanne wanne au watano watano. Nia ni kuwapa nafasi watoto wasalimiane na kujenga ukaribu kati yao.

Wasalimiane na waelezane habari za nyumbani kwao. Ikiwa kama kuna mmoja wao ana jambo la mafanikio fulani nyumbani, basi wengine wampongeze na kumtakia mema.

Kama mmoja wao ana msiba nyumbani, hao wengine wampe pole na wamwombee nguvu katika hiyo hali ngumu.

Ningeendelea kufanya hivyo kwa wiki nzima hata mwezi mzima.

Lengo ni kuwafanya wanafunzi wawajali wenzao, wawaheshimu wenzao na wajihusishe na wenzao hasa katika hali za shida na changamoto za maisha.

Baada ya wiki moja au zaidi ningebadilisha hayo makundi ili wanafunzi wakutane na wengine wapya, hivyo kwamba kila mmoja anajenga ukaribu na uhusiano mzuri na wanafunzi wengine.

Nia ya kuwasaidia wanafunzi wajenge ukaribu kati yao na waone uzito wa kushirikiana, kuheshimiana na kusaidiani inatokana na ukweli kwamba utu wetu unajengwa katika matendo ya aina hiyo.

Binadamu mwenye utu ni yule anayewajali wenzake, hasa walio na shida, ni yule aliye tayari kumsaidia mwenzake katika changamoto za maisha. Hana ubinafsi.

Nimeona mfumo huu wa kufundisha somo la maadili katika nchi nyingine kama Finland ambapo wanafunzi wanajifunza mawazo mapya kwa vitendo hata kabla hawajapewa vitabu.

Badala ya kueleza maana ya neno “maadili”, mwalimu anawaelekeza wanafunzi kufanya matendo ya kiuadilifu mara nyingi akitumia mifano kama ilivyo hapo juu.

Si ajabu kwamba wanafunzi wataelewa maana ya maadili, si kutokana na maelezo ya mwalimu au ya kamusi, lakini kutokana na matendo yao wenyewe darasani. Matendo hunena kuliko maneno.

Hatua nyingine

Hatua inayofuata katika kufundisha somo hili darasa la tatu na la nne, ni kuwapa fursa ya watoto kusimulia mifano mizuri wanayoiona katika jamii zao.

Kwa mfano, mwanafunzi anaweza kusimulia jinsi jirani yake nyumbani anavyojitoa katika huduma za kijamii kama kuwasaidia maskini, kushiriki kazi za usafi katika kijiji au mtaa wao, na kadhalika.

Lengo hapa ni kuwafanya wanafunzi hawa wadogo waone na wathamini mifano mizuri ya uadilifu katika jamii zao.

Nimesema mara nyingi gazetini humu kwamba hakuna njia nzuri zaidi inayozidi mifano mizuri katika kufundisha.

Pia napendekeza kwamba somo hili, katika madarasa ya mwanzo, lisipangiwe mitihani ili wanafunzi wasiwe na msukumo wa kujifunza kwa kukariri ili wafaulu mitihani.

Somo hili likifundishwa vizuri litapendwa sana na wanafunzi. Kwa uzoefu wangu nimeona kwamba wanafunzi wanapenda somo hili na huwa wanalikumbuka miaka mingi baadaye.

Nimesikitika kumwona mjukuu wangu akiweka nguvu kubwa katika kukariri somo la maadili katika kitabu chake cha darasa la tatu.

Tuchukue maamuzi magumu kuepa kufanya wanafunzi wakariri somo la maadili.

Mwanafalsafa Albert Einstein (1879-1955) anasema: ‘’Lengo la elimu si kujilimbikizia tu maarifa mengi, ni kukuza uwezo wa kufikiri na kujenga utu katika mioyo ya wanafunzi.’’

Ikiwezekana pengine katika madarasa ya tano na sita, tunaweza kutoa mitihani katika somo la maadili, tukizingatia kwamba mfumo wa kukariri haufai katika kutoa elimu bora.

Kama mimi ni mwalimu wa somo hili katika maradasa haya, ningewataka wanafunzi waandike insha kuhusu matendo ya uadilifu wanayoyaona katika familia zao na jamii zao.

Nia ni kuchokoza mioyo yao, si uwezo wao wa kukariri. Hakuna mtu anayekariri kwamba ukiona mwenzako ana shida, na unaweza kumsaidia, basi na umsaidie.

 Hatuhitaji kukariri kwamba mwenye msiba anapewa pole, na anayeumwa anatembelewa nyumbani au hospitalini. Hizi ni nguvu za rohoni.

Ni muhimu kutambua kwamba tunapofundisha maadili tunajenga mioyo ya wanafunzi, si kuwaongezea maarifa.

Somo la maadili ni somo la kujenga mioyo, si somo la kujitayarisha kwa mitihani. Utu, uadilifu, ukarimu, heshima na kadhalika, ni tabia za roho kuliko uwezo wa kiakili.

Mtu anaweza kuwa na uwezo mkubwa wa akili na wa kukariri lakini asiwe na uwezo wa kumjali na kumheshimu mwenzake.

Tunaona mifano lukuki ya watumishi wa umma wenye uwezo mkubwa wa akili lakini si waadilifu.

Somo la maadili si somo la kukariri, ni somo la kujenga mioyo ya watoto na wanafunzi. Ni somo endelevu katika maisha.

Mwalimu wa somo la maadili aweke mazingira ya upendo na mshikamano darasani. Awapende na kuwajali wanafunzi wake.

 Tuzingatie kwamba mwanafunzi wa umri huu, kama vile watu wazima, anajifunza kwa mafanikio zaidi kutokana na yale anayoyaona kwa mwalimu kuliko anayoyasema mwalimu.

Mtaalamu wa elimu ya awali, Johann H. Pestalozzi (1747-1827), anasema: ‘’Mtoto anajifunza uadilifu kwa kuona uadilifu katika matendo kuliko katika somo au hotuba ya mwalimu au msemaji.’’

Prof. Raymond S. Mosha. Barua pepe:

(255) 769 417 886; (255) 783 417 886.