Noti za Waarabu zinavyozivuruga Yanga, Simba

Dar es Salaam. Simba na Yanga zimeonekana kutamba kwenye mashindano ya klabu Afrika katika kipindi cha miaka sita ya hivi karibuni jambo lililozifanya ziwe gumzo barani Afrika.

Hata hivyo wakati Yanga na Simba zikionekana kuleta ubishi katika mashindano ya kimataifa, bado zimeonekana kusumbuliwa na nguvu ya fedha ambayo timu nyingi kutoka Kaskazini mwa Afrika zimekuwa nayo kulinganisha na vigogo hivyo viwili vya Tanzania.

Katika kipindi hicho cha miaka sita, timu za Kaskazini zimeonyesha jeuri ya fedha kwa kung’oa baadhi ya wachezaji muhimu na makocha wa timu hizo kutokana na ushawishi wa kifedha ambao zimekuwa zikiwapa.

Makocha au wachezaji hao walijikuta wakiziacha kwenye mataa Simba na Yanga na kufuata mishahara minono Uarabuni.

Ifuatayo ni orodha ya wachezaji na makocha waliowahi kuzitumikia Yanga na Simba na kisha kufuata malisho ya kijani zaidi huko Uarabuni.

Luis Miquissone

Februari 23, 2021, Luis Miquissone alifunga bao la kideoni katika mechi ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly na  kuiwezesha Simba kupata ushindi wa bao 1-0.

Bao hilo liliifanya Al Ahly ivutike kumsajili Miquissone ambapo ilitoa dau la Dola 900,000 (Sh2.3 bilioni), dau ambalo Simba haikulikataa.

Clatous Chama

Dirisha kubwa la usajili kwa mwaka 2023 halikuacha furaha kwa mashabiki wa Simba kwani baada ya Miquissone kusajiliwa na Al Ahly, nyota mwingine wa timu hiyo, Clatous Chama naye aliondoka kwa kujiunga na RS Berkane ya Morocco.

Kiasi cha fedha kinachotajwa kufikia Sh 1.5 bilioni kilitumika na RS Berkane kuishawishi Simba iwauzie mchezaji huyo jambo ambalo lilitimia.

Sven Vandenbroeck

Noti za FAR Rabat ya Morocco ziliacha majonzi Simba baada ya timu hiyo kumbeba ghafla kocha wake mkuu, Sven Vandenbroeck ambaye alikuwa ametoka kuiongoza Simba kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2020/2021.

Japo kiwango cha mshahara ambacho alikipata AS FAR hakikutajwa, inasemekana kuwa Vandenbroeck alipata mshahara mkubwa zaidi ambao ulimshawishi kwenda Morocco.

Nasreddine Nabi

Baada ya kuiongoza Yanga kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu mara mbili mfululizo, Juni, 2023 kocha Nasreddine Nabi alifuata majani ya kijani zaidi Morocco ambako alienda kujiunga na AS FAR ambayo ilimpa maslahi bora zaidi.

Akiwa Morocco, Nabi aliiongoza AS FAR kumaliza katika nafasi ya pili.

Fiston Mayele

Mwaka huohuo, Yanga ilipata pigo lingine kufuatia kuondoka kwa mshambuliaji wake aliyekuwa moto wa kuotea mbali kwa kufumania nyavu, Fiston Mayele.

Mayele aliondoka baada ya Yanga kumuuza kwa Pyramids FC kwa dau la Sh2 bilioni.

Sead Ramovic

Baada ya kuitumikia Yanga kwa siku 82 tu, kocha Sead Ramovic amekumbwa na upepo wa noti za Waarabu baada ya kujiunga na CR Belouzdad inayoshiriki Ligi Kuu ya Algeria.

Mshahara wa Dola 40,000 kwa mwezi, umeonekana kumshawishi Ramovic aiache Yanga kwenye mataa na kwenda Algeria.