Mwisho wa M23 hauonekani DRC-5

Baada ya hali ya usalama kuzorota zaidi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), huku DRC na Rwanda zikishutumiana kuhusu msaada kwa waasi wa M23, wakuu wa mataifa ya Afrika Mashariki walikutana jijini Nairobi, Kenya, Juni 20, 2022, na kukubaliana kupeleka jeshi la kikanda DRC ili kujaribu kumaliza vita mashariki mwa nchi hiyo.

Wakuu hao walikubaliana kuanzisha jeshi hilo na kutoa wito wa kusimamishwa mapigano, ikiwemo kuondoa uhasama.

Ingawa kikosi hicho kitachangiwa na wanajeshi kutoka nchi za Afrika Mashariki, na pamoja na kwamba Rwanda nayo imo katika nchi za Afrika Mashariki, taarifa kutoka Kenya haikusema chochote kuhusu iwapo wanajeshi kutoka Rwanda watahusishwa kwenye jeshi hilo la kikanda.

Hata hivyo Serikali ya Congo imesisitiza kutokubali wanajeshi wa Rwanda katika jeshi hilo.

Mkuu wa Tume ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahmat, ameyakaribisha matokeo ya mazungumzo hayo, akisema anaomba utekelezwaji wa haraka wa maamuzi hayo ili kurejesha amani mashariki mwa Congo.

DRC yenye utajiri wa madini inapambana kufa au kupona kuyadhibiti makundi ya wanamgambo waliojihami kwa silaha mashariki mwa taifa hilo, mengi miongoni mwao yakiwa yametokana na vita viwili vya kikanda vilivyodumu kwa robo muongo uliopita.

Mapigano makali yaliyozuka hivi karibuni huko mashariki yamefufua uhasama wa muda mrefu kati ya Kinshasa na Kigali, huku DRC ikiilaumu jirani yake Rwanda kwa kurejea kwa kundi la waasi wa M23.

Hata hivyo, Rwanda imekuwa ikikana kuwasaidia waasi hao, huku mataifa hayo kwa pamoja yakishutumiana kwa kufanya mashambulizi yanayovuka mipaka.

Kwa kumalizia mfululizo wa makala hizi, ni vyema kujikumbusha mambo muhimu yanayohusu hili kundi la waasi la M23, ambalo limekuwa kiini cha mzozo usiokoma nchini DRC. Kundi hili pia linajiita Jeshi la Mapinduzi ya Congo.

M23 ni kundi la waasi lililoanzishwa na wanachama wa zamani wa kundi la wanamgambo wa Kitutsi, waliokuwa wanaungwa mkono na Rwanda na Uganda.

Hawa walikuwa wamejumuishwa katika jeshi la Congo chini ya makubaliano yaliyosainiwa Machi 23, 2009, kwa maelewano kuwa waweke silaha chini kama mojawapo ya masharti ya kushirikishwa katika siasa za DRC.

Kiini chake ni yale makubaliano waliyotiliana na Serikali Machi 23, 2009. Hiyo ndiyo siku ambayo kikundi kilichojiita ‘Chama cha Kitaifa cha Ulinzi wa Watu’ (CNDP) kilitia saini mkataba wa amani na Serikali ya DRC.

Baada ya kusaini mkataba huo, kikundi hicho kiliacha uasi na kuwa sehemu ya jeshi la serikali, huku CNDP ikibadilika kuwa chama cha kisiasa.

Lakini kwa nini kundi hili linaendelea na mapigano? Huenda ni vigumu kujua, lakini viongozi wa kundi hilo wanadai kuwa halitachoka kudai haki ya raia wa DRC na kutaka makubaliano ya mkataba yaliyofanyika Nairobi, Kenya, kutekelezwa baada ya yale ya Entebbe, Uganda, kushindwa.

Katika mkutano uliofanyika mjini Entebbe, Uganda, wajumbe wa DRC waliacha mazungumzo hayo baada ya kushindwa kukubaliana na maneno ya waraka ulionuiwa kukomesha rasmi uasi huo.

Msemaji wa Serikali, Lambert Mende, anasema: ” Uganda inaonekana kuwa na maslahi katika M23, jambo linaloifanya kuwa sehemu ya mzozo huo.” Wakati huo huo, hakuna tarehe za kuanza kwa mazungumzo zilizowekwa.

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, pia alishutumiwa kwa kuihujumu Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kutowaalika viongozi wa Burundi na Tanzania kwenye mazungumzo hayo.

Kiongozi wa chama cha upinzani cha Freedom and Unity Front, Jenerali David Sejusa, anasema: “(Museveni) alianzisha uasi huo. Aliwapa silaha, akawapa msaada wa fedha, akawapa vifaa na kuwapa sare. Kwa hiyo, si kama nazungumza nje ya nchi.” Ni kinyonga yeye. Anageuka kisha anajiweka kana kwamba yeye ndiye anataka kuleta amani.”

Baada ya mazungumzo ya Uganda kushindikana, Desemba 12, 2013, Serikali ya DRC na kundi la M23 walikutana jijini Nairobi, Kenya, na kutiliana saini mkataba wa amani uliokusudiwa kuleta maridhiano, uthabiti na maendeleo mashariki mwa nchi hiyo.

Licha ya makubaliano hayo, kulikuwa na ugumu wa kuleta amani na utulivu eneo hilo. Katika mwisho wa juma ulioangukia Desemba 14-15, takriban watu 21 waligunduliwa kuwa wamekatwakatwa mapanga hadi kufa katika eneo hilo, ingawa wahalifu hawakujulikana.

Zaidi ya hayo, Januari 2, 2014, Kanali Mamadou Ndala, aliyekuwa kamanda wa kikosi maalumu cha jeshi la DRC na aliyeongoza operesheni ya kuwasaka waasi mashariki mwa nchi, aliuawa katika jimbo la Kivu Kaskazini na kundi la waasi wa Kiislamu la Allied Democratic Forces lenye chimbuko lake nchini Uganda.

Msemaji wa kundi hilo, Meja Willy Ngoma, mara kadhaa anasema Serikali ya Rais Felix Tshisekedi imekataa kutekeleza mambo waliyokubaliana alipoingia madarakani, na badala yake anatuma wanajeshi wake kuwashambulia M23. Anasema mapigano ya hivi karibuni yanatokana na jeshi la DRC kuanza kile alichokiita ‘uchokozi’ badala ya kutimiza ahadi.

“Sisi tunajibu mapigo peke yake. Ni hao wamekuja kushambulia ngome zetu. Sisi tunajibu mapigo yao na kuwafukuza mbali kabisa,” anasema Meja Ngoma.

Kundi hilo lilianza vita dhidi ya Serikali ya DRC Aprili 2012, wakati huo Rais wa DRC alikuwa Joseph Kabila, likimshutumu kwa kuwatenga watu kutoka jamii ya Watutsi na kukataa kuheshimu mikataba ya amani iliyokuwa imefikiwa awali.

 Mkataba wa Nairobi ulifikiwa baada ya kundi hilo kupigwa na wanajeshi wa Serikali ya DRC wakisaidiwa na wanajeshi wa Umoja wa Mataifa.

M23 ni kundi lililoundwa Aprili 4, 2012, baada ya kuishutumu Serikali kushindwa kuheshimu mkataba wa amani uliokuwa umesainiwa Machi 23, 2009, na hivyo kuliita kundi lake M23 kama kifupi cha Machi 23.

“Tulikubali kusaini Mkataba wa Nairobi. Tulisaini tena Mkataba wa Kinshasa na Rais Félix Tshisekedi alipoingia madarakani baada ya mazungumzo ya miezi 14, na tukakubaliana kuhusu mambo mengi. Tunasubiri watekeleze mambo tuliyozungumza. Badala yake, wamekuja kushambulia ngome yetu. Sisi tunajibu mapigo yao,” anasema Meja Ngoma.

Kulingana na Meja Ngoma, wanataka Serikali ya DRC ifanye mazungumzo ya kitaifa kuhusu amani, waasi hao waajiriwe na kuruhusiwa kuhudumu katika Jeshi la Serikali (FARDC), wanasiasa wa kundi hilo washirikishwe kwenye Serikali, na Jeshi la Serikali lipambane na kushinda makundi mengine ya waasi kama Allied Democratic Forces (ADF).

Pia, wanasema walimwambia Rais Tshisekedi kwamba wako tayari kufanya kazi katika Jeshi la DRC, na kama Serikali imekataa, basi wako tayari kurudi vijijini kwa mapigano na kundi la ADF kwa sababu wanaona linaendelea kuua ndugu zao.

Anasema: “Hatupendi kupigana na Serikali ya Congo. Sisi tunataka amani, ndiyo maana tulisitisha mapigano ili tutafute na tujenge amani ndani ya Congo.”

Kulingana na Meja Willy Ngoma, wao M23 wanataka amani ya raia wote wa DRC bila ubaguzi wa aina yoyote na kwamba kila raia wa Congo anastahili kuwa huru ndani ya nchi yake.

“Hatutaki baadhi ya raia wa Congo wawe wa muhimu kuliko wengine. Tunataka makundi yote ya waasi kama ADF yaondoke Congo,” anasema Meja Ngoma.

Inavyoelekea, kama hakuna hatua madhubuti za kuchukuliwa kukomesha uasi unaoendelea DRC, haielekei kama uasi utaisha siku za karibuni, na huenda hali ikawa mbaya kuliko inavyoweza kufikiriwa.