
Dar es Salaam. Wakati kukiwa na makundi mbalimbali ya watu wanaohitaji msaada, Benki ya Maendeleo imetaja umuhimu wa hatua ya kurudisha kwa jamii kwa ajili ya ustawi wa jamii.
Benki hiyo, ambayo mwaka 2024 ilifanikiwa kutumia zaidi ya Sh180 milioni katika mbio za hisani, imetumia Sh140 milioni kununua vifaa katika wodi ya watoto njiti ya Hospitali ya Rufaa Kanda ya Kaskazini ya KCMC, iliyopo mkoani Kilimanjaro.
Akizungumza leo Jumatatu, Februari 3, 2025, Mkuu wa Idara ya Fedha wa benki hiyo, Nolasco Charles, amesema kipaumbele cha benki hiyo ni kuendeleza ukuaji wa kibiashara kupitia njia za kidigitali sambamba na kuikumbuka jamii ya Watanzania.
Aidha, amesema kuwa benki hiyo inatambua umuhimu wa wajasiriamali wadogo kuchangia ukuaji wa biashara ya mikopo ya benki hiyo, ambapo mikopo ya wajasiriamali wadogo iliongezeka kutoka Sh74 bilioni kwa mwaka 2023 hadi Sh88.7 bilioni kwa mwaka 2024.
“Licha ya wateja wa juu wanaokopa Sh3 bilioni na wengine wanaokopa Sh500 milioni, wajasiriamali wadogo wanaokopa Sh500,000 ndiyo wateja wakubwa waliyoiletea faida benki hii kwa kipindi cha miaka miwili mfululizo,” amesema Charles.
Charles amesema licha ya benki hiyo kuwa na leseni ya kanda, inaendelea na mchakato wa kukamilisha maombi ya leseni ya kuwa benki kamili ili ifungue matawi zaidi kote nchini.
“Ili uwe benki kamili, inabidi uwe na mtaji wa kuanzia Sh15 bilioni, na mpaka Desemba 2024 mtaji wetu umeongezeka kwa asilimia 15 na kufikia Sh21.9 bilioni. Hivyo, tuna kila sababu ya kuwa benki kamili yenye matawi yake,” amesema.
Mjasiriamali Amina Juma amesema, licha ya benki hiyo kutoa mikopo yenye riba nafuu, huduma za haraka wanazozipata wakati wanapohitaji msaada zimekuwa za kuridhisha.
“Hatupati shida tukihitaji huduma, lakini pia tunawashukuru kwa kutupatia mikopo midogo inayoendana na biashara zetu za chakula,” amesema Amina.