
Dar es Salaam. Shirika la Uwezo Tanzania limeanisha maeneo saba yanayopaswa kufanyiwa mabadiliko katika Sera ya Elimu ya Mwaka 2014, toleo la 2023, iliyozinduliwa jana Jumamosi, Februari mosi, 2025, huku likitoa mapendekezo ya kinachopaswa kufanyika.
Upungufu ulioainishwa umegusa maeneo ya utangulizi na hali ya sasa, kutambua mabadiliko ya kimataifa, mfumo, miundo, na utaratibu ulioboreshwa wa elimu na mafunzo kwa viwango bora.
Pia, upatikanaji wa fursa za elimu na mafunzo, usimamizi na uendeshaji wa elimu na mafunzo, umuhimu, maono, shabaha, na malengo ya sera, mfumo wa elimu na mafunzo unaozingatia masuala mtambuka.
Serikali ilifanya mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Tanzania ya mwaka 2014 na kuja na Toleo la 2023 ikiwa imelenga kuwezesha vijana wanaomaliza ngazi mbalimbali za elimu kuwa na uwezo wa kujiajiri kwa kuwapatia mafunzo yanayoendana na karne ya sasa ya 21.
Kufuatia hilo, Shirika la Uwezo Tanzania kupitia Mkurugenzi Mtendaji wake, Baraka Mgohamwende, leo Jumapili, Fabruari 2, 2025 limefanya uchambuzi wa sera hiyo iliyozinduliwa jijini Dodoma, huku likisema mabadiliko hayo ni hatua muhimu katika kujumuisha ujuzi wa karne ya 21 na msingi wa kujifunza.
Hata hivyo, amesema inahitaji mikakati madhubuti ya utekelezaji, mageuzi ya mafunzo kwa walimu, na mifumo ya tathmini iliyo wazi ili kuhakikisha wanafunzi wanapata maarifa yanayowiana na mazingira halisi ya maisha.
Mgohamwende ameweka wazi kuwa, ingawa sera inatambua mabadiliko ya kiteknolojia, kiuchumi, na kijamii kama vigezo vya mageuzi ya elimu, haielezi wazi jinsi ujuzi utavyopatikana na kutathminiwa.
Katika eneo la mfumo, miundo, na utaratibu ulioboreshwa, amesema sera inasisitiza elimu jumuishi, kuhakikisha wanafunzi wote wanapata elimu ya msingi, huku utangulizi wa njia mnyumbuliko za kujifunza unapendekeza mfumo wa elimu unaojumuisha nadharia na vitendo ili kuhakikisha uwiano kati ya maarifa ya kitaaluma na ujuzi wa kiutendaji.
“Muundo wa elimu ya msingi bado ni wa kawaida. Mfumo huu unaendelea kulenga zaidi mitihani badala ya kuhimiza fikra bunifu na utatuzi wa matatizo.
“Pia, kuna ujumuishaji hafifu wa mafunzo ya ufundi. Ingawa sera inazungumzia mafunzo ya ufundi, haijaweka mkakati wa kina wa jinsi ujuzi huo utavyopandikizwa katika elimu ya awali,” amesema.
Katika elimu na mafunzo kwa viwango bora, sera inatilia mkazo Tehama kama nyenzo ya kuboresha ufundishaji, ujifunzaji, na upataji wa ujuzi huku ikilenga kuoanisha mtaala wa elimu na mahitaji ya soko la ajira na maendeleo ya taifa.
Hata hivyo, sera haijaeleza jinsi walimu watafundishwa kufundisha fikra tunduizi, ubunifu, na maarifa ya kidijitali,” amesema.
Katika hilo, amesema kuna pengo katika mbinu za kufundisha mawazo bunifu na ubunifu, ingawa elimu ya sayansi na teknolojia imepewa kipaumbele, ila sera haijaweka mwongozo wa wazi wa jinsi ubunifu, uongozi, na uwezo wa kuhimili mabadiliko vitakavyojumuishwa katika mtaala.
Upatikanaji wa fursa mbalimbali za elimu na mafunzo pia ni eneo lililoguswa, huku ikieleza kuwa sera inahimiza fursa sawa za kujifunza, ikiwemo kwa wanafunzi wenye ulemavu na wanafunzi wa kike katika masomo ya STEM.
“Lakini ujumuishaji wa ujuzi ni mdogo kwa kijamii, ingawa inahimiza upatikanaji wa elimu, sera haijaweka bayana jinsi ujuzi wa kijamii kama vile ushirikiano, uongozi, na ustahimilivu unavyopaswa kuingizwa katika elimu,” amesema.
Kuhusu upanuzi wa njia mbadala za kujifunza kwa kuanzisha programu za kujifunza kwa njia huria na masafa, kuboresha upatikanaji wa elimu na ujifunzaji wa maisha yote, ila kuna mtazamo mdogo wa ujasiriamali, wakati ambapo sera haitilii mkazo wa kutosha kuhusu ujasiriamali kama sehemu ya elimu ya msingi.
Eneo lingine lililoguswa ni namna sera inavyotambua haja ya kuwa na walimu wenye ujuzi wa kutosha kwa ajili ya mfumo wa elimu unaozingatia umahiri, huku ikisisitiza ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi ili kuboresha ubora wa elimu na upatikanaji wake.
“Hata hivyo, katika hili, mgawanyo wa majukumu katika maendeleo ya walimu, majukumu ya taasisi za mafunzo ya walimu hayajaelezwa kwa kina, hali inayosababisha mapengo katika kuwaandaa walimu kwa ujuzi wa karne ya 21.
Pia kuna mkakati dhaifu wa uhakiki wa ubora, na hakuna mfumo wazi wa kupima jinsi ujuzi wa karne ya 21 unavyofundishwa na kutathminiwa,” amesema.
Kwenye elimu ya mazingira, sera inajumuisha elimu ya mabadiliko ya tabianchi kwa kuwafundisha wanafunzi kuhusu uendelevu na uhifadhi wa mazingira, huku ikigusia elimu ya afya (Ukimwi/VVU) na ustawi kwa kujumuisha elimu ya afya na ustawi, inayoendana na ujuzi wa uraia wa kimataifa.
“Lakini kuna ukosefu wa mafunzo ya afya ya akili na akili hisia. Sera haijajumuisha mafunzo ya ustahimilivu wa kiakili, usimamizi wa msongo wa mawazo, na akili hisia, ambavyo ni ujuzi muhimu wa maisha katika karne ya 21,” amesema.
Eneo la umuhimu, maono, shabaha, na malengo, amesema sera imejikita katika falsafa ya kujitemea kwa kuendelea kutilia mkazo elimu ya kujitegemea, ili kuhakikisha wanafunzi wanaandaliwa kuajiriwa na kujiajiri, huku ikiweka msisitizo wa kuwajengea wanafunzi ubunifu, uwezo wa kuchambua mambo, na matumizi ya teknolojia.
“Ila hakuna mpango wa upimaji kwani sera imeainisha mipango mipana, ila hakuna mipango mahsusi na hatua za kuchukuliwa au kuingiza stadi za karne ya 21 katika mipango ya somo, maandalio ya masomo, na tathmini ya wanafunzi au upimaji,” imesema.
“Hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya sera na mahitaji ya ajira ya miaka ijayo. Sera haijaonyesha wazi mabadiliko yanayolenga mifumo ya soko la ajira la siku zijazo, kama vile matumizi ya akili bandia, mifumo otomatiki, na uchumi wa kidijitali.
Wakati walimu wenye ujuzi stahiki ikiwa ni eneo lililoguswa katika uchambuzi huu, Rais Samia Suluhu Hassan alipokuwa akihutubia kabla ya kufanya uzinduzi rasmi aliahidi Serikali itaendelea kuajiri walimu wenye sifa na kuwapa mafunzo stahiki ili waendane na mwenendo wa sera mpya ya elimu iliyozinduliwa.
“Pia tutapitia upya maslahi ya kada ya ualimu nchini ili kuipa hadhi inayostahiki kada hii kama mama wa taaluma zote duniani,” alisema Rais Samia.