
CEASIAA Queens ya Iringa katika dirisha hili dogo imeongeza wachezaji wanne kwenye maeneo tofauti.
Timu hiyo iko nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi ikicheza michezo tisa ushindi mechi tatu, sare moja na kupoteza tano ikikusanya pointi 10.
Akizungumza na Mwanaspoti, kocha wa timu hiyo, Ezekiel Chobanka alisema wachezaji hao watatumika kwenye mchezo na Simba baada ya vibali vyao kukamilika.
Wachezaji hao ni Annastazia Baltazar, Elizabeth Edward, Zuhura Bakari na Anita Adongo kutokea Kenya.
Chobanka alisema ongezeko la wachezaji hao litaongeza ushindani kwenye kikosi chake ambacho kinapambana kumaliza ndani ya nafasi nne za juu.
“Nadhani mechi yetu na Simba tutakuwa na wachezaji wote walioingia dirisha dogo, ni mchezo wa kucheza kwa tahadhari kubwa kutokana na aina ya mpinzani tunayekutana naye ni mgumu,” alisema Chobanka.