Bosi mpya Pamba Jiji kuanza na mambo haya

OFISA Mtendaji Mkuu wa Pamba Jiji, Peter Juma Lehhet amesema mojawapo ya malengo yake makubwa ni kuhakikisha timu hiyo ya jijini Mwanza inasalia Ligi Kuu Bara msimu ujao, huku akiomba zaidi sapoti kwa wadau na mashabiki wa kikosi hicho.

Akizungumza na Mwanaspoti, Peter alisema licha ya mikakati mingi iliyopo ndani ya kikosi hicho ila jambo kubwa analoanza nalo ni kuinusuru isishuke Ligi Kuu Bara, huku akieleza hataki kuona Pamba ikirudia tena kushiriki Ligi ya Championship.

“Hii ni nafasi nzuri kwetu ya kusahihisha na kuepusha aibu ya Kanda ya Ziwa, tulichukua muda mrefu kupanda Ligi Kuu Bara sasa hatutaki kuona tunarudi huko, niwaombe kila mmoja wetu kwa nafasi yake tuzidi kuisapoti sana timu yetu,” alisema.

Peter ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Tehama Halmashauri ya Jiji la Mwanza, huku pia akikaimu Ukurugenzi wa Halmashauri ya jiji hilo, alisema atafanya kazi kwa ushirikiano na viongozi wenzake huku akiahidi kuzingatia weledi kwa kila mmoja wao.

“Nimepewa mikakati na Mkuu wa Mkoa, Said Mtanda ambaye pia ni mlezi na mshauri wa timu yetu, naahidi kutekeleza tena kwa vitendo, ingawa kama nilivyosema mwanzoni kudumisha umoja na mshikamano ndio silaha ya kufikia malengo tuliyojiwekea.”

Peter aliteuliwa wiki iliyopita na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda wakati wa chakula cha usiku na wachezaji, benchi la ufundi, viongozi na wadau wa timu hiyo, iliyofanyika jijini Mwanza, kwa lengo la kukinusuru kikosi hicho msimu huu.

Awali nafasi hiyo ilikuwa inakaimiwa na Ezekiel Ntibikeha ambaye pia ni meneja wa kikosi hicho na imepita takribani miezi minane, tangu aliyekuwa ofisa mtendaji mkuu, Alhaji Majogoro kuondolewa kisha kuteuliwa nafasi ya mjumbe wa bodi.

Pamba iliyorejea Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya kupita miaka 23 tangu iliposhuka daraja mwaka 2001, inashika nafasi ya 14 na pointi zake 12, baada ya kushinda michezo miwili tu, sare sita na kupoteza minane kati ya 16 iliyocheza hadi sasa.

Timu hiyo ambayo wikiendi iliyopita mlezi wake na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda alifichua baadhi ya wachezaji, wamekuwa wakibeti na tayari ameanza kuchuku hatua kuwashughulikia, itashuka uwanja wa ugenini keshokutwa Jumatano kucheza na Dodoma Jiji mchezo wa Ligi Kuu Bara.