KONA YA MAUKI: Ifahamu Migogoro ya kihaiba na namna ya kuitatua

Kwa kawaida, popote haiba mbili tofauti zinapogongana lazima mgogoro hutokea, ingawa hali hii inaweza kupunguzwa au hata kuepukwa kabisa.

Kwa kuiangalia migogoro, watu wanaweza kugawanywa katika aina kuu nne ambazo ni mchakatuaji, dikteta, haiba yenye asili ya huruma na haiba yenye asili ya msukumo.

Asili ya mchakato

Mtu huyu huwa mwenye akili ya uchambuzi wa mambo, mtu ambaye huwazia juu ya kazi inayofanywa zaidi ya watu wanaoifanya. Hupenda kuweka msisitizo katika michanganuo ya vitu na wakati wote anapenda awe na taarifa halisi ya kila kitu.

Siyo watu wa kupenda kuonana au kukutana sana na watu, kwa hali hii anaweza akakutumia ka barua kadogo tu, au akaridhishwa na meseji za simu zaidi hata ya kuonana ana kwa ana.

Faida yao pia ni watu walio sahihi katika yale wafanyayo, wanajipanga vema na kujiandaa na hii hufanya ufanisi wao kuwa juu.

Tatizo huonekana wenye kufikiri sana katika kila kitu na hii hufanya wengine kutowapenda.

Ukitaka kupatana na mtu wa haiba hii, basi ongea taarifa za tafiti mbalimbali, zenye takwimu na uhalisia, siyo porojo zenye umbea.

Mara nyingine huonekana wasumbufu, hasa kwa mafundi maana hupenda kila kazi ifanywe wakiwepo, ili waone muunganiko wa vitu na vitu vinavyofanywa ili wajifunze.

Dikteta (haiba yenye sili ya mabavu)

Mtu huyu ana asili ya ujeuri na ubabe, neno lake mara nyingi ni “mimi”, tena huwa na mfumo wa kidikteta katika kila kitu.

Anataka kila kitu kifanyike anavyotaka yeye, mtu aliye na amri juu ya kila kinachoendela na kwamba yeyote mwingine ni wa kawaida tu.

Kwa sababu ya kuongea kila alichokuwanacho pasipo kupima, mara nyingine huumiza wengine, hasa wale anaowaona kuwa wanyonge. Ana muda mchache sana na mambo ya watu zaidi anaangalia matokeo ya vile anavyohitaji vifanywe.

 Kama wewe ni mtu anayependa vitu vifanyike chap chap, basi huyu ndio mwenza wako wa kuwa naye. Ni mtu anayependa kufikia lengo alilojiwekea, na asiye na shaka hata kidogo juu ya hilo. Tatizo ni kwamba, katika kufikia lengo huwatawanya watu wote waliokaribu yake kwa maneno makali, matusi, kujitapa na majigambo. Watu wa haiba hii ni wababe wa maneno pia, wanaweza kumuumiza yeyote katika kutaka kwao kazi ifanyike vile wapendavyo wao.

Siyo tu kuwa wanafikiri kwamba mawazo yao au njia zao ni nzuri zaidi, bali pia hufikiri kwamba mawazo na njia zao ni za kipekee na hakuna mwingine aliyesawa nao. Hupenda kulazimisha mambo na pia kutawala wengine, ni watu walio washindani katika kila kitu.

Ikiwa unataka kumshughulikia mtu wa jinsi hii, basi yakupasa ujipange vema na kuhakikisha taarifa au madai uliyonayo dhidi yake yana ukweli na nguvu.

Mara utakapojaribu kumjibu kwa jeuri utajikuta unaumia wewe mwenyewe na mwisho wa siku yeye ndiye atakayegeuka mshindi.

Haiba yenye asili ya msukumo

Ni mtu mwenye kiasi cha ujeuri katika asili yake, lakini anayependa kuwa karibu na watu zaidi ya profesa au dikteta. Ni mtu mwenye kipawa katika mambo mengi na kiu ya kuwa maarufu na kukubaliwa na watu.

Ni mtu mwenye nishati na msukumo wa kufanya mambo na husukumwa na uchu alionao katika kuhakikisha mambo yanakwenda.

Ingawa ana nguvu na nishati tele, tatizo ni mgumu kuvumilia hadi mwisho atakapofikia malengo yake, na mambo yake kufikia mwisho.

Kwa sababu ya msukumo wake wa kufanya kazi, anaweza kuwashawishi wengine katika utendaji, mara nyingine hufuraia kuchangia mawazo na kushiriki katika utendaji wa mawazo yale yaliyotolewa.

Ni kiu na raha yake watu wampende na kuridhishwa naye na kwa hali hii huwa na kipawa cha kuweza kudumisha mahusiano, urafiki, uvumilivu na ucheshi. Ili kushughulika na watu hawa, huna budi pia kuwa mwenye msukumo wa ndani ili mtiane moyo katika kufikia mwisho mwema wa kila mlichokipanga.

Haiba yenye asili ya huruma

Ni mtu mpole, mwema mwenye kujali watu, hupatana na wale wasio na haraka ya kufanya mambo. Mtu wa watu, na mtu anayependa kupendwa. Anapouliza “unaendeleaje?” ni kweli kuwa haulizi tu kama salamu, bali anataka kujua jibu.

Mara zote hupenda kutoa msaada ingawa anaweza kuchelewa kutoa maamuzi.

Ni mtu aliye na tabia ambayo kwa hali yoyote ni vigumu kugombana naye.

Ingawa mtu wa aina hii siyo kiongozi mzuri, lakini ni mtu mzuri kuwa naye upande wako, ni mtu anayetia moyo na kujishusha.

Hata kama hawezi kuwa mstari wa mbele katika mambo, lakini ni mzuri katika kutia moyo na changamoto kwa wengine ili waendelee mbele. Anapokiamini kitu ni rahisi kuwahamasisha wengine pia.

Kama unataka kufaidi kutoka kwa mtu wa aina hii, kamwe usimkimbizekimbize, bali umsikilize kwa makini na kumuonyesha unampenda.