Simba, Yanga wa mjengoni kukiwasha Dodoma

Dodoma. Wabunge ambao ni mashabiki wa Simba na Yanga wanatarajiwa kuvaana kwenye mchezo mkali wa kirafiki utakaopigwa Jumamosi ijayo.

Benki ya Azania imetangazwa kuwa mdhamini mkuu wa Bunge Bonanza 2025 linayotarajiwa kufanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari ya John Merlin jijini Dodoma likihusisha wabunge na watumishi wa Bunge ambao wanashabikia klabu hizi.

Akizungumza katika makabidhiano ya vifaa, Mwenyekiti wa Bunge Bonanza Festo Sanga, amesema mgeni rasmi katika Bonanza hilo atakuwa Rais wa Shrikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia ambapo viongozi mbalimbali akiwemo Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Tulia Ackson watahudhuria.

Naye Meneja wa Azania Bank Tawi la Dodoma Liberia Peter ambao ndiyo wadhamini wa Bonanza hilo kwa mwaka huu alisema hii ni mara ya pili mfululizo benki hiyo inadhamini bonanza hilo la wabunge kwa kuwa benki hiyo inatambua umuhimu wa michezo na afya bora kwa wawakilishi wao, ili mwisho wa siku waweze kutimiza majukumu yao ya kuisimamia serikali kwa ufasaha.

“Tumetoa vifaa vyote vya kuwezesha bonanza hilo zikiwemo jezi, track suits,tisheti, medali pamoja na mipira, kwa kifupi tumefadhili kila kitu kitakachowezesha bonanza hilo kufanyika, ikiwemo hafla ya chakula cha jioni kwa wabunge itakayofanyika kwenye eneo la bunge siku hiyo.

 “Kwa mara nyingine mtashuhudia bunge bonanza lililoandaliwa kwa kiwango cha juu sana na tunatarajia bonanza la mwaka huu litakuwa zaidi ya lile tulilofanya mwaka jana kutokana na aina ya maandalizi ambayo tumeyafanya,” alisema Peter.

Wabunge hawa wamekuwa wakicheza mechi hii kila mwaka na limekuwa ni bonanza lenye msisimko wa hali ya juu na kufuatiliwa na watu wengi kutokana na uwezo ambao umekuwa ukionyesha na baadhi ya mastaa kama, Mwigulu Nchemba, Festo Sanga, Cosato Chumi na Anthony Mavunde.