Arsenal yafuzu, City hatarini kushuka daraja

London, England. Arsenal imeungana na Liverpool na Barcelona kufuzu hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya juzi kuichapa  Dinamo Zagreb mabao 3-0, huku Manchester City ikiwa hatarini kushuka daraja.

Tayari timu nane zimeshafuzu hatua ya 16 Bora ya michuano hiyo mikubwa Ulaya huku Manchester City ikiwa hatarini baada ya kulala mabao 4-2 dhidi ya PSG.

Huu ni msimu wa kwanza wa michuano hiyo ambayo inaendeshwa kwa mfumo mpya ambapo timu nane zimeshafuzu, huku timu inayomaliza kuanzia nafasi ya tisa hadi ya 24 ikitakiwa kucheza mtoano play-offs ambapo nane zitafuzu 16 Bora.

Timu nyingine ambazo zina nafasi ya kufuzu hatua hiyo ni, Aston Villa, Atalanta, Atletico, Bayern, Brest, Celtic, Dortmund, Feyenoord, Inter, Juventus, Leverkusen, Lille, Milan, Monaco na Real Madrid

Wakati huko mambo yakiwa hivyo, Manchester City inatakiwa kuhakikisha kuwa inapata ushindi kwenye mchezo wa mwisho wakati ikivaana na Club Brugge ili iwe na uwezekano wa kuingia kwenye mtoano ambapo timu 16 zitapambana kwenye mechi za nyumbani na ugenini kupata timu nane nyingine.

Timu  ambazo zinapewa nafasi kubwa ya kuwa kwenye mtoano ni Monaco, Feyenoord, Lille, Brest, Borussia Dortmund, Bayern Munich, Real Madrid, Juventus, Celtic, PSV, Club Brugge, Benfica, PSG, Sporting Lisbon na Stuttgart.

Manchester ilikutana na kichapo hicho ambacho kilikuwa kibaya zaidi kwa Pep Guardiola ambaye awali aliamini kuwa kikosi chake kinaweza kufanya vizuri kwenye mechi hiyo na kufufua matumaini.

Kwa sasa City ipo nafasi ya 25 kati ya timu  36 na imebakiza matumaini ya kucheza mchezo wa mwisho na kupata ushindi kama inataka kubaki kwenye michuano hiyo.

“Tumecheza vibaya, nafikiri kama hatutashinda mchezo wa mwisho basi hatuwezi kuwa na matumaini ya kufuzu na nafasi yetu itakuwa imeishia hapo,” alisema Pep Guardiola.

Endapo itapoteza mchezo wa mwisho, litakuwa pigo kwa City ambayo ilitwaa ubingwa huo mwaka 2023.