Hospitali ya Kamal Adwan huko Gaza inakabiliwa na uhaba wa maji na oksijeni

Wizara ya Afya ya Palestina imetangaza kuwa, Hospitali ya Kamal Adwan iliyoko kaskazini mwa Ukanda wa Gaza inakabiliwa na uhaba wa oksijeni na maji kutokana na mashambulizi makubwa ya ndege za kivita za jeshi la utawala wa Kizayuni.

Wizara ya Afya ya Palestina ilitangaza jana Ijumaa kuwa mashambulio ya makombora na mabomu yaliyolenga hospitali ya Kamal Adwan yamesababisha kuharibiwa kwa jenereta kuu la umeme la hospitali hiyo na kutoboa matangi ya maji; na kwa sababu hiyo, hospitali hiyo inakabiliwa na uhaba mkubwa wa oksijeni na maji jambo ambalo linahatarisha sana maisha ya wagonjwa na wafanyakazi wanaohudumu ndani ya hospitali hiyo.

Wizara ya Afya ya Palestina imeongeza kuwa, kushambuliwa hospitali ya Kamal Adwan kumesababisha kujeruhiwa wafanyakazi sita wa huduma za tiba wa hospitali hiyo, na hali za baadhi yao ni mbaya.

Sambamba na kulaani kitendo cha jinai cha jeshi la Kizayuni dhidi ya hospitali ya Kamal Adwan, wizara hiyo imeyataka mashirika ya kimataifa na ya kibinadamu kuisaidia hospitali hiyo na wafanyakazi wa sekta ya tiba katika Ukanda wa Gaza.

Wakati huohuo, Wizara ya Afya ya Gaza imetangaza kuwa: tangu vilipoanza vita vya Gaza tarehe 7 Oktoba 2023, idadi ya Wapalestina waliouawa shahidi hadi sasa imefikia 44,056 na idadi ya waliojeruhiwa imefikia 104,268.