
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu inakaribisha hatua yoyote ya kuuondolea kinga utawala wa Kizayuni na kuiwajibisha Israel kwa jinai zake za kivita na mauaji ya kizazi huko Palestina.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Iran Press, Esmail Baghaei amesema hayo kwenye mtandao wa kijamii wa X na kusema kuwa hatua ya Mahakama ya Kimataifa ya kutoa waranti wa kutiwa mbaroni watenda jinai wawili wakuu yaani waziri mkuu wa Israel na waziri wa vita wa utawala huo katili ni hatua nzuri.
Amesema: Iran inakaribisha hatua yoyote ya kufanikisha uadilifu na kukomesha kinga unayopewa utawala wa Kizayuni kutokana na mauaji ya umati na jinai za kivita na khiyana kwa ubinadamu huko Palestina na katika sehemu nyingine yoyote.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameongeza kuwa, kuchelewa kuchukuliwa hatua utawala wa Kizayuni ambapo moja ya sababu zake kuu ni ukwamishaji wa wazi na wa siri wa Marekani ambayo imeapa kuulinda utawala wa Kizayuni kwa hali yoyote ile ndiko kulikopelekea kuendelea na kuongezeka jinai za kutisha za Israel katika ardhi za Palestina.