Kitanzi kipya Man City, Newcastle United

London,England. Maisha huenda yakawa magumu kwa Manchester City na Newcastle United katika Ligi Kuu England (EPL) kwa siku za usoni hasa katika ununuzi wa wachezaji wa gharama kubwa na uendeshaji wa timu hiyo.

Hiyo inafuatia uamuzi wa klabu 16 zinazoshiriki Ligi hiyo kupiga kura kuidhinisha mabadiliko ya sheria zinazosimamia mikataba ya kibiashara, licha ya upinzani kutoka kwa Manchester City, Newcastle United, Nottingham Forest na Aston Villa.

Katika mkutano uliofanyika London, Ijumaa, klabu zilichukua muda usiozidi dakika 30 kuidhinisha mabadiliko ya kanuni za Miamala ya Vyama Vilivyohusishwa (APTs) kwenye ligi hiyo.

Klabu 16 zilipiga kura ya kuafiki huku nne zikipinga zikiwemo Manchester City na Aston Villa ambazo kabla ya mkutano huo zilishawishi klabu nyinine ili kutafuta uungwaji mkono.

Kwa mujibu wa kanuni za EPL, ili mabadiliko yaidhinishwe, angalau klabu 14 za Ligi Kuu zinahitajika kupiga kura ya ndio.

Kura ya Ijumaa ilikuja baada ya jopo huru kubaini vipengele vya sheria za Ligi Kuu kuwa kinyume cha sheria mapema mwaka huu, kufuatia kesi iliyochochewa na Manchester City.

Sheria za APT ziliundwa na Ligi Kuu ili kuzuia klabu kunufaika kutokana na mikataba ya kibiashara au ya udhamini na makampuni yanayohusishwa na wamiliki wao ambayo inachukuliwa kuwa juu ya “thamani ya soko inayostahili”.

Ligi Kuu ilisema mabadiliko ya kanuni yanahusiana na “kuunganisha tathmini ya mikopo ya wanahisa” na “ni pamoja na kuondolewa kwa baadhi ya marekebisho yaliyofanywa kwa sheria za APT mapema mwaka huu”.

“Madhumuni ya sheria za APT ni kuhakikisha klabu haziwezi kufaidika na mikataba ya kibiashara au punguzo la gharama ambazo hazina thamani ya soko kwa sababu ya uhusiano na vyama vinavyohusika,” ilisoma taarifa ya Ligi Kuu.

Vyanzo vya habari vimefichua kwamba wawakilishi kutoka Chelsea na Manchester United wote walizungumza kwenye mkutano kabla ya kura, wakizitaka klabu kupiga kura kupitisha mabadiliko hayo.

Mwakilishi wa Manchester City alikataa kuzungumza.

Manchester City ndio wanaonekana watakuwa wahanga wakuu wa sheria hiyo kwani shirikala ndege la Etihad ambalo ni mdhamini wake mkuu, lina uhusiano na mmiliki wa timu hiyo, Sheikh Mansour.

Kwa muda mrefu, Manchester City imekuwa ikituhumiwa kuwa inatumia kivuli cha udhamini kuchota hela kwa siri kutoka kwa mmiliki wake.

Hali hiyo ni kama ilivyo kwa Newcastle United ambayo mmiliki wake, Yasir Al-Rumayyan kutoka Saudi Arabia naye anahusishwa na kampuni ya Sela ambayo inaidhamini timu hiyo kwa tangazo lake kukaa kifuani kwenye jezi ya timu hiyo.