
Kocha wa Manchester City Pep Guardiola, amesema alikuwa amepanga huu uwe msimu wake wa mwisho na timu hiyo, lakini ameamua kuongeza mkataba mwingine kwa kuhofia kuiangusha timu hiyo baada ya kupoteza michezo minne.
Man City haina matokeo mazuri msimu huu, ikiwa hadi sasa inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu nyuma ya vinara Liverpool.
Guardiola ambaye ameshatwaa ubingwa wa Ligi Kuu England mara sita amekubali kusaini mkataba wa miaka miwili, awali mkataba wake na timu hiyo ilikuwa unamalizika mwishoni mwa msimu huu na wengi waliamini kuwa anaachana na timu hiyo.
“Kuanzia mwanzoni mwa msimu huu nimekuwa na mawazo mengi, kuhusu mustakabali wa mkataba wangu, awali nilikuwa nafikiri kuhusu mkataba wangu na niliona kuwa huu ni mwaka wangu wa mwisho.
“Lakini kutokana na matokeo ambayo tumekuwa nayo hivi karibuni zaidi mwezi uliopita, niliona kuwa huu siyo muda wangu wa kuondoka kwenye timu hii nafikiri kuwa sasa siyo muda mzuri wa kuondoka kwenye timu hii.
“Naona kuwa vichapo mara nne ni sababu ya kwanza mimi kubaki kwenye timu hii, naona kuwa klabu hii bado inanihitaji sana, na naamini kuwa bado tupo pamoja kuendeleza mazuri ya hii timu,” alisema kocha huyo raia wa Hispania.
City imepoteza michezo minne, ilichapwa dhidi ya Bournemouth na Brighton, pia ililala kwa mabao 4-1 dhidi ya Sporting Lisbon ambayo ilikuwa inafundishwa na kocha wa sasa wa Man United Ruben Amorim,ilitupwa nje kwenye michuano ya Carabao na Tottenham yakiwa ni matokeo mabaya kwa timu hiyo tangu Pep alipojiunga nayo.