
Dar es Salaam. Shirika la Reli Tanzania (TRC) limesema ndani ya miezi minne limesafirisha zaidi ya abiria 1,000,000 kupitia treni yake ya kisasa ya SGR, ikiwa ni zaidi ya mara mbili ya waliokuwa wanasafirishwa na treni za zamani kwa mwaka.
Taarifa iliyotolewa leo Jumatano Novemba 20, 2024 na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano, Fredy Mwanjala imesema; .
“Shirika limefanikiwa kusafirisha abiria zaidi ya 1,000,000 katika kipindi cha miezi minne tangu uzinduzi wa njia za treni za umeme kati ya Dar es Salaam na Dodoma mnamo Juni 2024.
“Idadi hiyo ni mara mbili ya abiria waliosafirishwa na treni ya zamani (MGR), ambayo ilisafirisha jumla ya abiria 400,000 katika kipindi cha mwaka mmoja,” imesema na kuongeza taarifa hiyo.
Pia, TRC imesema inatambua umuhimu wa huduma hiyo ya kisasa katika kuboresha usafiri, kuongeza ufanisi wa biashara na kutoa chaguo la haraka na salama kwa abiria na hivyo imewataka wananchi kuilinda miundombinu ya reli hiyo.
Novemba 14, 2024 Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), Augustino Vuma akikagua mradi huo pamoja na wajumbe wengine alisema zaidi ya Sh20 bilioni zimekusanywa tangu uanze.
“Tumeona katika taarifa zao TRC wametueleza hadi sasa zaidi ya Sh20 bilioni zimekusanywa tangu imeanza kutoa huduma za kusafirisha abiria kupitia treni ya kisasa ya SGR.
“Mapato yatokanayo na abiria huwa ni asilimia ndogo lakini asilimia 80 na zaidi mara nyingi inatokana na usafirishaji wa mizigo, kama haya yaliyopatikana ni asilimia 20 tunaamini mizigo ikianza wafanyabiashara wengi watatumia fursa hiyo na mapato ya shirika yataongezeka,” alisema na kuongeza Vuma.
Safari za treni hiyo zilianza rasmi Julai 14, 2024 kwa Dar es Salaam na Morogoro kisha baadaye kuongezwa za Dar es Salaam na Dodoma.