Mwanahistoria wa Israel: Sasa ni wakati wa vikwazo vya kimataifa dhidi ya Tel Aviv

Katika mahojiano na gazeti la El Pais la Uhispania, mwanahistoria wa Israel, Ilan Pappé amesema kuwa “mauaji ya kimbari ya Gaza yanafanywa na utawala unaoamini kuwa umepata fursa ya kihistoria ya kuiangamiza Palestina” na amesisitiza kuwa: “Sasa ni wakati wa kuwekwa vikwazo vya kimataifa dhidi ya Tel Aviv.

Akielezea kile kinachotokea sasa huko Gaza, Ilan Pappé amesema: Maelezo pekee ya sera za Israel katika Ukanda wa Gaza ni kwamba mauaji ya kimbari. Sio tu kwa sababu ya idadi kubwa ya wahanga wa mauaji hayo, ambao wengi wao ni wanawake na watoto, lakini pia kwa sababu itikadi ya nyuma ya vitendo hivi inayoamini kwamba wakazi wote wa Gaza na labda Wapalestina wanapaswa kuangazwa.”

Akijibu swali na mwandishi habari wa El Pais aliyeuliza kwamba ‘miezi kadhaa iliyopita uliandika makala ukisema Uzayuni unaporomoka’, bado unashikilia msimamo huu? mwanahistoria huyo wa Kiisraeli amesema: “Ndiyo, nimebainisha michakato kadhaa ambayo, kwa pamoja, inaweza kuangusha Uzayuni kama itikadi, na mchakato huu umeongezeka tangu nilipoandika makala hiyo.”

Pappé ni profesa katika Kitivo cha Sayansi ya Jamii na Utafiti wa Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Exeter, Uingereza, na ni mkuu wa Kituo cha Ulaya cha Utafiti wa Palestina cha chuo hicho. Ameandika vitabu kadhaa kikiwemo kile cha The Ethnic Cleansing of Palestine.