Makazi ya Netanyahu yarushiwa moto, inadhaniwa ni hujuma ya wapinzani wake wa ndani

Mapema usiku wa kuamkia leo, moto umerushwa katika makazi ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, huko Caesarea, tukio lililoelezwa kuwa ni “kuongezeka kwa hatari.”

Uchunguzi wa pamoja umeanzishwa baina ya shirika la usalama wa ndani la Shin Bet na polisi wa eneo hilo. Ripoti zinasema moto huo umetua katika ua wa nyumba ya Netanyahu.

Hakuna uharibifu ulioripotiwa katika tukio hilo na taarifa ya pamoja kutoka vyombo vya usalama imesisitiza kuwa Netanyahu na familia yake hawakuwa nyumbani wakati huo.

Polisi na Shin Bet pia wamesema wameanzisha uchunguzi kuhusu tukio hilo na kueleza kuwa “linaashiria kuongezeka kwa hatari.” 

Inaonekana kuwa wahusika wa hujuma hiyo ni wapinzani wa Netanyahu ndani ya Israel.

Kushindwa kwa jeshi la Israel kufikia malengo yake wakati huu vita vikiendelea huko Gaza na Lebanon, na kufeli kwa malengo ya kukombolewa mateka wa utawala huo wanaoshikiliwa na harakati za mapambano ya ukombozi wa Palestina kumesababisha upinzani mkubwa wa ndani kwa Benjamin Netanyahu.