Jumatatu, 18 Novemba, 2024

Leo ni Jumatatu tarehe 16 Jamadul-Awwal 1446 Hijria mwafaka na tarehe 18 Novemba 2024.

Siku kama ya leo miaka 1165 iliyopita alifariki dunia Abu Hanifa Dinawari, mtaalamu wa fasihi, nujumu na mwanahisabati wa Kiislamu. 

Abu Hanifa Dinawari ni mmoja wa wanafalsafa na wataalamu wa theolojia na wanahisabati wa zamani wa ulimwengu wa Kiislamu ambaye alizaliwa mjini Kermanshah yapata mwaka 222 Hijiria. Alikuwa msomi mashuhuri katika kipindi cha utawala wa Samanid huku akitabahari katika elimu za nahw, lugha, mantiki, nyota, elimu ya maumbo, uhandisi na kadhalika.

Mbali na hayo pia Abu Hanifa Dinawari alikuwa mtaalamu wa elimu ya mimea, historia, jografia, nyota, hisabati na kadhalika. Moja ya athari maarufu za mwanazuoni huyo ni pamoja na ‘Kitaabun-Nabaat’ ambacho kimejikita katika kutambua mimea, ‘Al-Akhbaaru al-Twiwaal’ ‘Al-Faswaahah’ ‘Al-Shiiru wa Al-Shuaraa Wal-Buldaan.’

Katika siku kama ya leo miaka 237 iliyopita Louis Daguerre mchoraji, mvumbuzi na mtaalamu wa elimu wa fizikia wa Kifaransa alifariki dunia.

Mwaka 1789 mtaalamu huyo alifanikiwa kuvumbua mambo kadhaa. Miongoni mwa uvumbuzi muhimu wa Louis Daguerre ni ule wa mwaka 1839 ambapo alifanikiwa kuvumbua camera ya kupigia picha na kwa kutumia camera hiyo akapiga picha ya kwanza iliyokuwa ikionekana vizuri.

Louis Daguerre

Siku kama ya leo miaka 185 iliyopita ilianza awamu ya pili ya mapambano ya wananchi wa Algeria wakiongozwa na Abdul Qadir bin Muhyiddin dhidi ya ukoloni wa Ufaransa.

Ufaransa iliivamia Algeria mwaka 1830 ikiwa na nia ya kuikalia kwa mabavu nchi hiyo. Amir Abdul Qadir akiwa pamoja na wapiganaji elfu 50 alipambana na wakoloni wa Kifaransa hadi mwaka 1847. Lakini hatimaye jemedari huyo wa Algeria alishindwa na kukamatwa mateka.

Karibu karne moja baadaye, baada ya Vita vya Pili vya Dunia, wananchi wa Algeria walianzisha tena mapambano ya kupigania uhuru dhidi ya wakoloni wa Kifaransa na mwaka 1962 Algeria ilipata uhuru.

Abdul Qadir bin Muhyiddin

Siku kama ya leo miaka 121 iliyopita ulitiwa saini mkataba wa Mfereji wa Panama kati ya Marekani na Jamhuri ya Panama.

Kwa mujibu wa mkataba huo mfereji huo ulikodishwa milele kwa Marekani mkabala wa Panama kupewa dola milioni 10 taslimu na dola laki mbili na nusu kila mwaka. Baadaye wananchi wa Panama walianzisha mapambano ya kupinga mkataba huo na hatimaye wakailazimisha Marekani kutazama upya kipengee cha kukodishwa mfereji huo milele.

Kwa msingi huo mwaka 1978 Jimmy Carter na Jenerali Omar Efraín Torrijos viongozi wa wakati huo wa Marekani na Panama walitia saini mkataba mpya ambao kwa mujibu wake mfereji wa Panama ulirejeshwa chini ya mamlaka kamili ya nchi hiyo mwishoni mwa mwaka 1999.

Miaka 68 iliyopita na katika siku kama ya leo yaani tarehe 18 Novemba mwaka 1956, nchi ya Morocco ilipatia uhuru.

Kabla ya hapo ardhi hiyo ilikuwa chini ya tawala na mataifa mbalimbali. Hata hivyo kufuatia kuenea dini Tukufu ya Kiislamu katika maeneo mbalimbali duniani, yakiwemo maeneo ya kaskazini mwa Afrika, ardhi ya Morocco nayo ikawa miongoni mwa ardhi za utawala wa Kiislamu.

Mwaka 1921 Ufaransa iliidhibiti Morocco hadi mwaka 1956 wakati nchi hiyo ilipojitangazia uhuru.

Siku kama ya leo miaka 62 iliyopita alifariki dunia msomi na mwanafizikia wa Denmark, Niels Bohr, akiwa na umri wa miaka 82.

Bohr alizaliwa mwaka 1885 na kuvutiwa mno na elimu ya hisabati. Msomi huyo alifanya uchunguzi na uhakiki mkubwa katika elimu hiyo. Niels Bohr pia alifanya uhakiki katika masuala ya atomu na mwaka 1945 alitunukiwa Tuzo ya Nobel katika medani ya fizikia kutokana na uvumbuzi wake katika masuala ya atomu.

Niels Bohr

Katika siku kama ya leo miaka 61 iliyopita kanali Abdul Salam Arif alishika hatamu za uongozi nchini Iraq baada ya kufanya mapinduzi ya umwagaji damu.

Ikulu ya Rais na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iraq zilishambuliwa kwa mabomu na kupelekea kuuawa Abdul Karim Qasim aliyekuwa Rais wa nchi hiyo. Itakumbukwa kuwa, Abdul Karim Qasim naye aliingia madarakani mwaka 1958 baada ya kufanya mapinduzi ya umwagaji yaliyohitimisha utawala wa Kifalme nchini humo.

Abdul Salam Arif

Katika siku kama ya leo miaka 11 iliyopita kundi la kigaidi na kitakfiri la Batalioni ya Abdullah Azzam lililokuwa likiongozwa na gaidi Msaudi Arabia, Majid al Majid ambalo ni miongoni mwa matawi ya kundi la kigaidi la al Qaida, lilishambulia ubalozi wa Jamhuri ya Kislamu ya Iran mjini Beirut huko Lebanon kwa kutumia magaidi wawili waliojilipua kwa mabomu.

Katika mashambulizi hayo mawili ya kigaidi watu 23, akiwemo Hujjatul Islam Walmuslimin Ibrahim Ansari aliyekuwa Mwambata wa Utamaduni wa Jamhuri ya Kislamu ya Iran nchini Lebanon na mke wa mmoja kati ya wanadiplomasia wa Iran, waliuawa shahidi na watu wengine zaidi ya 160 walijeruhiwa.

Walinzi wanne wa ubalozi wa Iran mjini Beirut pia waliuawa katika hujuma hiyo ya kigaidi. Baada ya hujuma hiyo ya kigaidi, Majid al Majid alitiwa nguvuni lakini aliuawa kwa njia ya kutatanisha akiwa katika hospitali ya kijeshi mjini Beirut kabla ya kutoa taarifa yoyote na maiti yake ikakabidhiwa kwa maafisa wa utawala wa Saudi Arabia.

Hujjatul Islam Walmuslimin Ibrahim Ansari