Bila vigezo hivi Grammy hutoboi

Dar es Salaam. Baada ya kuwepo kwa minong’ono mingi katika mitandao ya kijamii kuhusiana na tuzo za muziki nchini Marekani zinazokwenda kwa jina la Grammy kuwapendelea na kuwanyonya baadhi ya wasanii, sasa Mwananchi imekusogezea baadhi ya vigezo vya kuwasilisha kazi Grammy.

1.Kuwa na mwanachama (kutoka Grammy) mwenye haki ya kupiga kura katika Recording Academy

Kabla ya kuingiza wimbo au albamu yako unatakiwa kuhakikisha kuwa una wanachama wengi zaidi wa kukupikia kura ili pindi utakapoingiza kazi zako basi hao ndio watakaokusukuma ili uweze kuingia katika kinyang’anyiro hicho.

Mbali na kuwa na wanachama lakini pia utatakiwa kuanza kuhudhuria mikutano ya Grammy ya ana kwa ana pamoja na ile inayofanyika kwenye mitandao ili kujua taratibu na sheria za tuzo hizo.

2.Kufanya maandalizi mapema (miezi 12-24) kabla ya Grammy
Hakikisha wimbo unaochagua kuingia katika kinyang’anyiro hicho unakuwa bora kwani wanachama wa ‘Recording Academy’ wanahimizwa kupigia kura muziki kwa kuzingatia ubora, si umaarufu.

Lakini pia waandaji wa tuzo hizo wanashauri wanaoingiza nyimbo zao kwa mara ya kwanza kufanya utafiti wa kategori pamoja na kuomba ushirikiano au kuwauliza washindi wa tuzo hizo wa nyuma.
 
Aidha msanii anatakiwa kuwa na timu iliyonyooka asitumie bajeti kubwa kwenye kurekodi, anatakiwa kuhifadhi kiasi kikubwa cha bajeti ili kuajiri washauri, wasimamizi, mapromota, wataalamu, au maajenti wa masoko ambao watakakusaidia kuendesha kampeni za kupigiwa kura katika hatua ya kwanza ya Grammy iitwayo ‘For Your Consideration’.

3.Kutoa ngoma mapema, na kuweka mkakati madhubuti wa kuusambaza muziki wako

Kama mwaka huu tuzo hizo zimekupita basi unatakiwa kutazamia kwa mwaka mwingine ambapo utatakiwa kutoa ngoma kuanzia sasa kufanya promosheni, kusambaza muziki kwa lengo la kuweka attention kwenye mitandao ya kijamii na platform mbalimbali ili iwe rahisi baadaye kuingiza katika tuzo hizo.

4.Kufanya kampeni katika hatua ya kwanza ya kupigiwa kura ‘For Your Consideration’

Baada ya kuingiza wimbo wako katika hatua hiyo ya kwanza na Grammy ikakubali basi unachotakiwa ni kuanza kufanya kampeni kwa kuwajulisha wanachama wenye haki ya kukupigia kura waweze kukupigia raundi ya kwanza.

Mbali na hilo pia utatakiwa kufungua tovuti iitayo FYC ambapo msanii utatakiwa kuweka vitu vyako kadhaa ikiwemo video za nyuma ya pazia za wimbo wako, historia fupi kuhusu muziki wako, wasifu wako kama msanii, orodha ya timu na washiriki.

Lakini pia katika tovuti hiyo hupaswi kuingiza vitu kama kuweka maneno ya kashifa kutoka kwa msanii mwingine, kutumia nembo ya Grammy lakini pia kuwahonga wapiga kura.

Mbali na hayo pia hakikisha wimbo utakaopendekeza kuingia katika tuzo hizo utatakiwa kuwa na matokeo kwa jamii, mfano kupitia mwanamuziki kutoka Nigeria, Yemi Alade wimbo wake wa Tomorrow umepenya kutokana na kuitia moyo jamii ambayo imekata tamaa.