Mripuko wa bomu wa kando ya barabara waua watu 3 katika mji mkuu wa Somalia

Askari wawili na raia mmoja wameuawa na wengine watatu wamejeruhiwa katika mripuko wa bomu uliotokea kando ya barabara katika mji mkuu wa Somalia wa Mogadishu jana Jumatano.

Ali Ahmed, afisa wa usalama wa mji mkuu Mogadishu amethibitisha habari hiyo na kusema kuwa, shambulio hilo limetokea katika kitongoji cha Daynile cha Mogadishu na limesababishwa na mripuko wa bomu lililokuwa limetegwa kando ya barabara.

Watu wengine watatu wamejeruhiwa katika mripuko huo na kupelekwa hospitalini kwa matibabu.

Ameongeza kuwa jeshi la polisi na askari wa vyombo vingine vya usalama walifika eneo la tukio na kuanza uchunguzi mara moja.

Genge la Al-Shabaab ambalo tangu mwaka 2007 linaendesha mauaji na mashambulizi ya kigaidi nchini Somalia limedai kuhusika na shambulio hilo.

Itakumbukwa kuwa, mwishoni mwa mwezi uliopita wa Oktoba, Wizara ya Ulinzi ya Somalia ilisema kwamba, jeshi la nchi hiyo likisaidiwa na washirika wa ndani na wa kimataifa, limefanya operesheni za kijeshi dhidi ya genge la kigaidi la Al-Shabaab na kuua magaidi zaidi ya 95 wa genge hilo.

Luteni Sheikh Abukar Mohamed, msemaji wa wizara hiyo, alisema katika mkutano na vyombo vya habari mjini Mogadishu kwamba, magaidi 45 waliuawa na vijiji vitatu vilikombolewa wakati wa operesheni ya kijeshi huko Shabelle ya Kati mwishoni mwa mwezi huo wa Oktoba 2024 na wengine waliuawa kwenye maeneo mengine.