Wagonjwa wenye maumivu makali kutibiwa kwa teknolojia ya tundu dogo

Dar es Salaam. Wagonjwa wenye maumivu ya mwili kwa muda mrefu yanayochangiwa na magonjwa mbalimbali, majeraha ya upasuaji au umri mkubwa sasa wanaweza kupata tiba katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) pasipo kufanyiwa upasuaji.

Mbali ya matibabu hayo kwa teknolojia ya tundu dogo, wagonjwa wameonywa kuhusu matumizi holela ya dawa za kupunguza maumivu.

Kwa mujibu wa hospitali hiyo, matibabu ya tundu dogo hufanyika kwa kutumia mtambo maalumu kuweka dawa na kuziba mshipa unaoleta changamoto ya maumivu ndani ya mwili.

Tayari watu 200 wenye maumivu ya muda mrefu wamejitokeza hospitalini hapo katika kambi ya matibabu iliyoanza  Novemba 4, 2024 ikitarajiwa kufikia tamati Novemba 15, 2024, huku wagonjwa 25 wameshapatiwa matibabu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 13, jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Profesa Mohamed Janabi amesema kambi hiyo imefanyika kwa kushirikiana na Dk David Prologo wa Hospitali ya Emory Johns Creek ya nchini Marekani.

Dk Prologo ni daktari bingwa wa tiba ya radiolojia aliyejikita kwenye matibabu kwa wagonjwa wenye maumivu makali.

“Mara nyingi watu huchukulia maumivu kama si ugonjwa, yapo yanayoathiri afya, mtu anapokuwa na maumivu makali anaathiri afya ya akili, sasa matibabu yapo tunachofanya ni kuziba mshipa wenye tatizo. Tayari kupitia kambi hii wagonjwa 25 wamepatiwa matibabu na wengine 186 wanaendelea na hatua mbalimbali za uchunguzi,” amesema.

Profesa Janabi amesema kutokana na maumivu makali ya muda mrefu, wapo watu wametengeneza utegemezi wa dawa za kupunguza maumivu kitendo ambacho huwatumbukiza kwenye maradhi ya figo.

Dawa za maumivu zinapotumika kiholela hutengeneza tatizo la figo, ambalo Profesa Janabi amesema dawa hizo ni sababu mojawapo ya wagonjwa wa figo kufika hospitalini hapo.

“Wagonjwa wa figo tunaowapokea ni wale waliokumbwa na matatizo ya sukari, presha na wale wanaotumia holela dawa za kupunguza maumivu, endapo mtu mwenye maumivu ya muda mrefu hatapata tiba atadumu na maumivu hayo maisha yake yote,” amesema.

Amesema kwa wanaopatiwa matibabu hospitalini hapo hawana haja ya kuyarudia kwa kuwa tatizo hutatuliwa mara moja.

Kuhusu gharama amesema hutofautiana kati ya wagonjwa akieleza wapo wanaotibiwa kwa punguzo la gharama, msamaha, wengine fedha taslimu au kutumia bima ya afya.

Mkuu wa Idara ya Radiolojia MNH, Dk Frederick Lyimo amesema matibabu ya kuondoa maumivu mwilini hufanyika kwa wagonjwa ambao kwa muda mrefu wameshindwa kupata tiba.

Amesema miongoni mwa tiba ambazo hutolewa ni sindano kuua neva kwa matibabu ya maumivu ya tumbo yasababishwayo na saratani ya kongosho, maumivu ya nyonga au mabega na sindano za uti wa mgongo na goti.

Dk Prologo amesema kupitia kambi hiyo ya siku 10 wamekutana na wagonjwa 200 wenye maumivu sehemu mbalimbali za mwili, huku 25 wamepatiwa tiba.

Amesema ili matibabu hayo yawe endelevu lazima madaktari waliopewa mafunzo kuendeleza huduma hiyo.