
Licha ya kuwepo matamko mbalimbali ya viongozi wa Serikali na wale wa CCM kuhusu yaliyotokea katika chaguzi za 2019 na 2020, bado tumerejea kwenye malalamiko yaleyale kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa unaoendelea nchini.
Awali, kulikuwa na malalamiko hasa ya vyama vya upinzani katika chaguzi zilizopita, yakiwamo ya wagombea wao kuenguliwa kwa sababu zinazotajwa kutokuwa na mashiko na kuwepo kwa upendeleo kwa wagombea wa CCM.
Kwamba, wagombea wa upinzani wanaenguliwa, halafu wakienda kukata rufaa wanakuta ofisi zimefungwa.
Wizara ya Nchi katika Ofisi ya Rais, Tamisemi inayosimamia uchaguzi huo haichukui hatua yoyote kwa wanaofunga ofisi, badala yake wakata rufaa wanaambiwa waende kwa mkurugenzi wa halmashauri au katibu tawala wa mkoa au katibu mkuu wa wizara hiyo.
Mizunguko yote hii kwa wagombea maana yake nini kama sio hujuma kwa wagombea wa upinzani?
Malalamiko hayo yalijirudia pia hata katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, ambapo pia wagombea wa upinzani wengi walienguliwa.
Kutokana na malalamiko hayo na mfumo mzima wa uchaguzi unaolalamikiwa kutotenda haki kwa vyama vya upinzani, CCM ilishinda kwa kishindo katika chaguzi hizo.
Kwa kuzingatia malalamiko hayo, baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuingia madarakani Machi 2021 alianza kufanya mageuzi ya kisiasa, kijamii na kiuchumi.
Katika siasa alikutana na vyama vya siasa katika mkutano ulioandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa Desemba 2021 na baada ya mkutano huo, Rais Samia aliunda kikosi kazi kwa ajili ya kupitia hoja zilizozungumzwa katika kikao hicho.
Baada ya kikosi kazi hicho kutoa mapendekezo yake Oktoba 21, 2022, kilichofuata tuliona ni ujio wa miswada mitatu ya sheria za uchaguzi ambazo ni Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani na Sheria ya Vyama vya Siasa.
Hata hivyo, sheria hizo zililalamikiwa kutokidhi mahitaji ya kupatikana kwa uchaguzi ulio huru na wa haki na hasa uhuru wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.
Rais Samia akionyesha kutaka maridhiano zaidi, alikuja na falsafa yake ya R nne (4R) anazozitumia katika utawala wake. 4R maana yake ni maridhiano (Reconciliation), mabadiliko (Reforms), ustahimilivu (Resilience) na kujenga upya (Rebuilding).
Akizungumza katika mkutano mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo uliofanyika Mlimani City Dar es Salaam, Machi 5, 2024, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM-Bara, Abdulrahman Kinana aliyemwakilisha Rais Samia, aliwahakikisha Watanzania kwamba uchaguzi wa serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 utakuwa huru na haki.
Alisema pia, Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali wana dhamira ya dhati ya kuhakikisha mchakato huo unakuwa huru na haki ili watu wapate fursa ya kuwachagua viongozi wanaotaka.
“Niwahakikishie, Rais Samia ameamua uchaguzi wa mwaka huu na ujao unakuwa huru na haki, ninazungumza hili nina uhakika wapo wenye shaka na kauli hii, lakini wanazo sababu zinazotokana na mwaka 2019 na mwaka 2020,” alisema.
Baada ya kauli na hatua hizo zote, leo tunasikia malalamiko yaleyale ya unyanyasaji wa wagombea wa upande mmoja.
Kurejewa kwa malalamiko haya maana yake sasa juhudi zile zimeshindikana na pengine sasa kinachotafutwa ni kusaka ushindi wa CCM, liwalo naliwe.
Awali, kuna baadhi ya vyama na wadau wengine walitilia shaka juhudi hizo. Wasiwasi ulizidi pale Serikali iliposema imesogeza utekelezaji wa mchakato wa mabadiliko ya Katiba miaka mitatu mbele, ambapo katika kipindi hicho itakuwa ikitoa elimu ya Katiba kwa wananchi.
Malalamiko haya katika uchaguzi huu ni mwendelezo wa malalamiko yaliyodumu kwa zaidi ya miaka 30 tangu mfumo wa vyama vingi uliporejeshwa mwaka 1992.
Serikali ya CCM ililaumiwa kupoka madaraka ya kidola, yakiwamo ya kuwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano ambaye pia ni mwenyekiti wa chama hicho mwenye madaraka makubwa mno.
Matokeo yake ndio haya, tunakuwa na uchaguzi shaghalabaghala. Uchaguzi unasimamiwa na Ofisi ya Rais Tamisemi, waziri mwenyewe kada wa CCM, unatarajia nini?
Huyo huyo ndiye anayesimamia wakurugenzi wa halmashauri, wakuu wa mikoa na wilaya na watendaji wa kata.
Huko kote mgombea wa upinzani akienguliwa atakuwa na nguvu gani ya kukata rufaa?
Kwa hali hii hatutarajii kuwa na uchaguzi mkuu ulio huru wala wa haki ifikapo mwaka 2025.