
Mwanza. Wakati ugonjwa wa usugu wa vimelea dhidi ya dawa (Uvida) ukitabiriwa kuongoza kwa vifo duniani ifikapo mwaka 2050, watoto wachanga chini ya mwezi mmoja na wale njiti wanatajwa kuwa miongoni mwa makundi manne yaliyopo hatarini kuupata.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), ugonjwa huo husababisha vifo vya watu 700,000 kwa mwaka, likitabiri hadi kufikia mwaka 2030 unaweza kusababisha vifo vya watu milioni 10 kila mwaka.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu, Novemba 11, 2024 katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Sayansi za afya na Tiba Shirikishi (Cuhas), mkurugenzi wa masomo ya uzamili na uzamivu chuoni hapo, Profesa Jeremiah Seni amesema tatizo hilo limeendelea kuongezeka duniani na mwaka 2014, zaidi ya watu 700,000 walifariki dunia kutokana na ugonjwa huo, lakini mwaka 2019 idadi ya waliofariki dunia iliongezeka na kufikia milioni 1.2.
Profesa Seni ambaye pia ameshiriki kutengeneza mpango mkakati wa kitaifa wa kukabiliana na usugu wa vimelea ulioanza mwaka 2017 na unaendelea hadi 2028, amesema tafiti zilizofanyika Cuhas zimeonyesha tatizo hilo linaathiri zaidi watoto chini ya mwezi mmoja, watoto njiti, wagonjwa waliofanyiwa upasuaji na wagonjwa waliopo vyumba vya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu.
Amesema watoto chini ya mwezi mmoja wanapata vimelea hao kupitia kwenye kitovu ambacho kinakuwa wazi baada ya kuzaliwa iwapo hakitofanyiwa usafi ipasavyo.
“Hawa vimelea wakiingia kwenye mfumo wa damu wanasababisha maambukizi. Huo ni ugonjwa unaosababisha madhara makubwa. Mtoto anapozaliwa, sehemu ya kitovu huwa wazi, hivyo kama usafi haupo vizuri vimelea wataingia na kwenda kwenye damu na kusababisha madhara,”amesema.
Profesa huyo ameeleza watoto njiti nao wapo hatarini kwa kuwa kinga yao ya mwili haijaimarika ukilinganisha na watoto wengine.
Akitaja sababu zinazochangia tatizo hilo, Profesa Seni amesema, “matumizi yasiyo sahihi ya dawa, lakini kuna sababu zinazotokana na mifumo yetu kwamba kuna baadhi ya maeneo bado hatuna uwezo wa uchunguzi na hii tunaongelea hospitali za wilaya kushuka chini…hospitali za mikoa na rufaa zenyewe uchunguzi upo vizuri.”
Amesema hali duni ya uchumi ni sababu nyingine ya usugu wa vimelea dhidi ya dawa, kwa kuwa baadhi ya watu wananunua dawa na kutumia bila uchunguzi na ushauri wa kitaalamu.
“Kuna tatizo pia la kiuchumi…kuna moja ya utafiti mkubwa umefanyika hapa (Cuhas) umeonyesha uhusiano wa moja kwa moja kati ya tatizo la usugu wa vimelea dhidi ya dawa na tatizo la umaskini kwa maana mtu hawezi kununua dawa za kutosha kumaliza dozi alizopangiwa kama ni siku tano au saba.
“Lakini pia umaskini ambao unasababisha mtu asiende kwenye vituo vya afya sababu ya gharama, hivyo kumeza dawa kwa dozi isiyotakiwa au kutumia dawa bila kufuata ushauri wa wataalamu au matokeo ya uchunguzi,” ameongeza.
Amesema kutokana na ugonjwa huo kuwa tishio, wanafunzi wawili wa chuo hicho watakaotunukiwa Shahada ya Uzamivu (PhD) Novemba 16, 2024 katika mahafali ya 17 ya chuo hicho, wamefanya utafiti wa uhusiano kati ya usugu wa vimelea vya dawa katika kundi la watoto na watu wenye virusi vya Ukimwi.
Awali, akizungumzia mahafali ya 17, Makamu Mkuu wa Cuhas, Profesa Erasmus Kamugisha amesema yataambatana na michezo, kongamano la kimataifa la sayansi na Naibu Waziri Mkuu, Doto Biteko anatarajiwa kuwa mgeni rasmi pamoja na mkutano mkuu wa mwaka wa wahitimu wa chuo hicho wa miaka iliyopita.