
Lindi. Chama Kikuu cha Ushirika Lindi Mwambao, kinachojumuisha Wilaya za Lindi, Kilwa na Mtama, kimeuza korosho zenye thamani ya Sh119 bilioni katika minada minne iliyopita.
Akizungumza katika mnada wa tano, leo Jumatatu, Novemba 11, 2024, Ofisa Masoko wa Chama Kikuu cha Lindi Mwambao, Glory Makele amesema mpaka kufikia mnada wa nne, korosho kilo 37,399,661 zimeuzwa kwa thamani ya Sh119 bilioni. “Tumeuza korosho kilo 37,399,661 na tumeshawalipa wakulima wote kwa minada mitatu. Kwa mnada huu wa tano, malipo yataanza kutolewa ndani ya wiki moja,” amesema Makele.
Makamu Mwenyekiti wa Lindi Mwambao, Hassan Mnumbe amesema katika mnada wa tano, korosho tani 3,171 zimeuzwa kwa bei ya juu ya Sh3,070 na bei ya chini ya Sh2,830.
Amebainisha kuwa mwaka jana walifanikiwa kuuza korosho tani 16,000 hadi mwisho wa msimu, lakini mwaka huu, kufikia mnada wa tano, tayari wameuza tani 30,000 wakivuka malengo yao ya ukusanyaji.
“Kutokana na mvua, korosho nyingi zimekuwa zikishushwa daraja hadi la pili, lakini tunashukuru kampuni ya TMX kwa kutusaidia kupata bei nzuri hadi sasa,” amesema Mnumbe.
Hawa Mchalagana, mkulima kutoka kijiji cha Nga’pa ameishukuru Serikali kwa kuwezesha bei nzuri ya korosho.
Amesema uzalishaji wa mwaka huu umekuwa mkubwa na bei nzuri, akisema hali ikiendelea hivyo, wakulima wa kusini watapata maendeleo makubwa.
“Zamani uzalishaji ulikuwa mdogo na bei ilikuwa ndogo, lakini sasa uzalishaji na bei vimeimarika, hali ikiendelea hivi, watu wa kusini hatutakuwa maskini tena,” amesema Mchalagana.
Jeby Salum, mkazi wa kijiji cha Nga’pa, ameishukuru Serikali kwa kuwasaidia wakulima kupata bei nzuri na kuharakisha malipo yao, akisema fedha wanazopata zinawawezesha kuwaandaa watoto wao kwa shule.
“Malipo tunayopata yanatusaidia kuwaandaa watoto kwa shule. Tunaishukuru Serikali kwa juhudi kubwa wanazofanya kwa wakulima wa korosho,” amesema Salum.