Anko Kitime: Kucheza muziki wa dansi na changamoto zake 

Dar es Salaam, Kwanza kabisa kuna changamoto ya msingi katika kuongelea uchezaji wa muziki wa dansi. Changamoto ya kwanza ni swali Je, Muziki wa dansi ni upi kwa siku hizi? Katika muziki wa taarabu kuna maendeleo ambayo yameleta kitu kinachoitwa Taradance, yaani Taarab yenye nia ya kuwainua watu wacheze dansi, tena mara nyingine Taarab hiyo huwa pia ina stage show.

Kisanii hilo ni jambo la kusifiwa kwani sanaa isipokuwa na mawazo mapya, hudumaa na pengine hata kufa, lakini katika makala hii hiyo ni moja ya changamoto.

Kuna muziki unaitwa Bongo Fleva huu ni mgumu zaidi kuuchambua kwani hata wenyewe wanaojinasibu kuwa ni wanamuziki wa Bongo Fleva, hushindwa kuelezea kwa ufasaha Bongo Fleva ni muziki wa aina gani, lakini katika muziki huo pia kuna kucheza sana.

Historia ya muziki wetu wa dansi inaenda sambamba na historia ya nchi yetu. Kwa ufupi muziki wa dansi ulianza haswa katika utawala wa Waingereza, hata neno dansi lilitokana na neno la Kiingereza ‘dance’, ni nyakati za utawala wa Muingereza alipoingiza utamaduni wa kuwa na klabu za dansi. 

Utamaduni huu awali ulikuwa ni wa kutumia santuri katika kucheza dansi. Santuri za awali zilikuwa pia zikiwa na maelezo kuwa wimbo husika ulikuwa ni wa mtindo gani, hivyo uchezaji wake ulieleweka. Mfano kulikuwa na mitindo kama Foxtrot, Waltz, na baadaye ikaja mitindo kama Chacha, Borelo, Rumba, Tango, Merengue, Twist na mingine mingi sana.  

Mitindo hiyo ilikuwa mahsusi na ilijulikana na kulikuwa hata na mafunzo ya namna ya uchezaji wake.  Kati ya vilabu vya awali vinavyokumbukwa ni klabu kutoka  Tanga iliyokuwa ikiitwa Young Noverty Dancing Club na  New Generation Dancing Club ya Dar es Salaam.

Klabu hizi zilikuwa na wacheza dansi maarufu ambao wakafikia hata kuanzisha mashindano ya dansi kati ya klabu mbalimbali. Klabu hizi ndizo zilileta chachu ya kwanza ya kuanzishwa kwa vikundi vya muziki ili wanachama wa klabu hizo wawe wanacheza muziki kutoka kwenye bendi badala ya santuri.

Vikundi vya muziki wa dansi vilizaliwa karibu katika kila mji mkubwa nchini. Kati ya vikundi vya awali vya jiji la Dar es Salaam ni Coast Social Orchestra na Dar es Salaam Social Orchestra, ambayo inasemekana ndiyo iliyokuwa mbegu ya kuanzishwa kwa Dar es Salaam Jazz Band, bendi ambayo nayo ilihamasisha bendi nyingi kuzaliwa.

Kwa miaka mingi bendi ziliendelea kujiendesha kwa mfumo wa klabu. Klabu zilikuwa na wanachama na waliogharamia kununua vyombo na mara nyingine hata kuwatunza wanamuziki ambao hawakuwa na ajira. 

Wanamuziki walijiunga na klabu na kuwa wanapiga muziki kama burudani kwa wanachama, bendi nyingi maarufu zilianzishwa kwa mfumo huo, kwa mfano Dar es Salaam  Jazz Band, Morogoro Jazz Band, Cuban Marimba Band na Jamhuri Jazz Band ambayo awali ilianza kama klabu ya vijana wa Kinyamwezi waliokutana Tanga kwenye mashamba ya mkonge na hivyo kuanzisha  Young Nyamwezi Club iliyokuja kuanzisha Young Nyamwezi Jazz Band hatimaye ikawa Jamhuri Jazz Band, katika kuenzi nchi yetu kuwa Jamhuri mwaka 1992. 

Katika kipindi hiki uchezaji wa muziki ulikuwa katika mpangilio ulioeleweka. Kabla ya kuanza wimbo wanamuziki walikuwa wakitangaza aina ya muziki ambao wanataka kuupiga, mfano bendi ilikuwa inatoa tangazo, ‘ Sasa bendi yenu inapiga muziki unaitwa Chiku na utapigwa katika mtindo wa Chacha’. Na hakika ulipoanza kupigwa muziki ule watu walijimwaga uwanjani na kushindana namna ya kucheza Chacha na si vinginevyo’.

Pia jambo jingine muhimu lilikuwa ni mavazi, kulikuwa na nguo maalumu za kuvaa unapoenda dansini, na hasa suti kwa kwa wanaume.

Kama ilivyo kawaida ya vijana popote duniani, mwanzoni mwa miaka ya 60 vijana wa kizazi kipya wa nyakati zile wakaingiza mtindo mpya wa uchezaji dansi kutoka Marekani, mtindo huo uliitwa twisti. Uchezaji wa twisti ulikuwa ni kunengua kwa kuzungusha visigino tofauti sana na twisti inavyochezwa siku hizi ambapo  kinachozungushwa ni kiuno. 

Lakini hata hivyo wazee wa miaka hiyo waliipiga vita sana twisti, kuna wanafunzi waliwahi kufukuzwa shule kwa kuonekana wanacheza twisti, mtindo ulioonekana kuwa ni uchezaji wa kihuni. 

Bendi nazo zilianza kubuni mitindo yake na kuanza kugundua aina za uchezaji wake, ikazaliwa mitindo kama, Msondo, Mundo, Segere, Dondola, Kiweke na kadhalika . 

Katika kucheza mitindo hii mipya kulikuwa na tofauti ya uchezaji kati ya wanaume na wanawake. Wanaume walicheza zaidi wakitikisa vifua vyao kuonyesha kuwa wao ni wanaume.

Katika miaka ya sabini, utamaduni wa bendi kuwa na ‘wacheza show’ ukaanza. Kwa vile utaratibu huu uliigwa kutoka bendi za Kongo. Hata uchezaji wake uliiga sana uchezaji wa Kikongo, ingawaje kulikuwa na bendi ambazo wachezaji wake walikuwa wabunifu na kuanza kugundua uchezaji wao na uchezaji huo ukawa unaigwa na wapenzi wa bendi hizo. 

Katika miaka ya karibuni kumekuwa kama hakuna tofauti kati ya uchezaji wa kiume na wa kike, unenguaji wa kiuno ambao zamani ilikuwa sifa hasa ya wachezaji wa kike, siku hizi si ajabu kabisa kukuta mwanaume akikatika kiuno kwa ufanisi  wa hali ya juu kuliko wanawake wenye asili yao. 

Na uchezaji huu wa kukata viuno kwa sasa  uko katika kila aina ya muziki kuanzia  taarab, dansi, singeli mpaka  Bongo Fleva.