Quincy Jones alinivutia kufanya kazi hii – Dr. Dre

Marekani, Mtayarishaji Muziki na Mkurugenzi Mtendaji wa Aftermath Entertainment, Dr. Dre  (59), amesema marehemu Quincy Jones ndiye aliyemvutia hadi kuingia katika fani hiyo iliyompatia mafanikio makubwa tangu miaka ya 1990.

Kauli ya Dr. Dre inakuja baada ya kifo cha Quincy Jones aliyefariki akiwa amezungukwa na familia yake mnamo Novemba 4 mwaka huu huko nyumbani kwake Bel Air, Los Angeles nchini Marekani.

Kulingana na Associated Press, Quincy Jones ambaye ni mkongwe katika utayarishaji muziki duniani na mtunzi wa nyimbo huku akishinda tuzo 28 za Grammy enzi za uhai wake, amefariki akiwa na umri wa miaka 91.

“Usiku wa leo tukiwa na moyo uliovunjika, tunalazimika kutangaza kifo cha baba na kaka yetu Quincy Jones. Ingawa ni habari ya kusikitisha katika familia yetu, tunasherehekea maisha mazuri ambayo aliishi na tunajua kamwe hakutakuwa na mwingine kama yeye.,’ taarifa ya familia ilieleza.

“Kwa kweli ni mtu wa aina yake na tutamkumbuka sana; tunapata faraja na fahari kubwa tukijua kwamba upendo na furaha ambavyo vilikuwa kiini cha nafsi yake, vilifurahiwa na ulimwengu kupitia vyote alivyovitengeneza. Kupitia muziki na upendo wake usio na kikomo, moyo wa Quincy Jones utaishi milele,” familia ilisema.

Ikumbukwe marehamu Quincy alifanyakazi na wasanii wakubwa na maarufu kama Tupac, Stevie Wonder, Michael Jackson, Snoop Dogg, LL Cool J, Sinatra, Tony Bennett, Lesley Gore,  Kanye West, Chaka Khan, Queen Latifah n.k.

Dr. Dre ambaye kupitia Aftermath Entertainment amefanya kazi na wasanii wakubwa duniani kama Eminem, Kendrick Lamar, Busta Rhymes, Snoop Dogg, The Game, 50 Cent n.k, kupitia ukurasa wake wa Instagram alizungumzia kifo cha Quincy.

“Quincy ndio sababu iliyonifanya niamue kuwa mtayarishaji wa muziki. Rekodi zake ndizo nilizotumia nilipoanza kazi hii,” aliandika Dr. Dre katika picha aliyochapisha akiwa na Quincy enzi za uhai wake.

“Wakati wote ambao nilitumia kuwa naye ulikuwa wa thamani na napenda jinsi alivyokuwa wazi, ushauri alionipa, mazungumzo tuliyokuwa nayo yamenisaidia katika maisha na kazi yangu. Milele nitahamasika na Quincy Jones asiye na kifani,” amesema  Dr. Dre.

Wawili hao walishirikiana katika mambo mengi kwa miaka mingi, Quincy alihudhuria kipindi cha redio cha Dre’s Beats1 The Pharmacy mwaka 2015, pia alikuwepo na Dre mwaka 2018 wakati Snoop Dogg alipopewa nyota yake ya heshima ya Hollywood Walk of Fame.

Utakumbuka Dr. Dree aliyetajwa na Jarida la Rolling Stone katika nafasi ya 56 katika orodha ya wasanii 100 bora duniani kwa muda wote, yeye na Snoop Dogg walishirikiana katika wimbo, Dr. Dre, Still D.R.E (1999) kutoka katika albamu ya pili ya Dr. Dre, 2001 (1999).

Wimbo huo ambao hadi Februari 2022 video yake ilikuwa imetazamwa (views) zaidi mara bilioni 1 YouTube na ndani ya mwaka huo kurejea tena katika chati ya Billboard Hot 100 na kushika nafasi ya 23, sio kwamba tu ulimfanya Dr. Dre kuwa rapa tishio, bali ulimtangaza zaidi Snoop Dogg.